The House of Favourite Newspapers

Marlaw: Wafanyabiashara Kariakoo Ndio Walinitoa Kimuziki

0

 

SEHEMU YA 7: KWENYE toleo la wiki iliyopita, Marlaw aliishia pale wakati akijaribu kuelezea namna alivyofanikiwa kutimiza lengo lake la kuingia studio na kukutana na watayarishaji wa muziki kisha wakamuelewa ubora wake na kumshirikisha kwenye moja ya nyimbo zao.

 

Huyu hapa tena Marlaw akiendelea kutujuza namna alivyopata hadi nafasi ya kutoa ngoma yake ya kwanza.

 

“KAMA nilivyosema baada ya kufanikiwa kufanya vizuri kwenye korasi ya Wimbo wa My Queen wa yule prodyuza Temu G na kuonekana nimewafurahisha wote kwa pamoja, palepale Temu G, aliniahidi kunipatia biti ili niingize ngoma yangu mwenyewe.

 

“Aliposema hivyo, moyoni mwangu nikafurahia sana na nikaamini sasa tayari lengo langu limetiki, hivyo na wao hawakukawia, mara moja Tuddy Tomas alikaa chini na kunipigia biti moja ambapo aliniuliza kama nina wimbo wowote nimuimbie tu hata korasi ili aone jinsi ya kuiweka sawa biti.

 

“Nikamwambia ninao kwani tayari kichwani nilikuwa na kile kikorasi cha wimbo wangu wa Bembeleza, hivyo bila kusubiri akaniambia niende kuandika ili aendelee kuiweka sawa hiyo biti.

 

“Kiukweli sikuweza kutoa hata nafasi ya kulala siku hiyo maana nilienda tu shule na usiku mzima nilikuwa naandika mashairi ya ngoma hiyo, kesho yake nilipompelekea ikiwa kamili hata yeye hakuamini.

 

“Nilipoenda aliniAmbia nijaribu, hivyo akapiga biti, kitendo cha kuimba kidogo tu mwenyewe aliridhika na kunitaka tuanze kurekodi palepale.

 

“Baada ya kutoka pale studio na kwenda shule, huwezi kuamini kuwa Tuddy na wenzake kwa kuwa walikuwa wakifanya kazi palepale redioni, walianza kuupiga ule wimbo lakini na sisi kishule shule tulikuwa tukiupiga sana na kutokana na mazingira ya wakati huo, Bembeleza ilitambaa ghafla tu pale shule pamoja na Iringa yote wakawa wameupenda sana.

 

“Kiukweli ulikuwa wimbo mzuri, ulitoka nje ya mipaka na kufika hadi Njombe Mjini na Mbeya kitu ambacho kilinifurahisha sana.

 

“Kuna mfanyabiashara mmoja wa pale Mbeya mara kwa mara alikuwa akichukua mzigo pale Kariakoo, hivyo katika safari zake kutoka Mbeya hadi Kariakoo jijini Dar, akaja kuwasikilizisha wenzake pale Kariakoo, wakamuuliza wimbo huo kaimba nani? Yule jamaa akawaelekeza kuwa mwenye wimbo huu ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtwango pale Njombe.

 

“Wakati huo nilikuwa kidato cha sita tena kipindi cha kuelekea likizo ambayo nikirudi tena shule namaliza masomo.

 

“Basi wale jamaa baada ya kuelezwa vile walilazimika kumuomba namba zangu za simu, bila kinyongo alizisaka na kuwapatia na wao bila kupoteza muda wakanipigia na kuniuliza kama kweli mimi ndiye mwenye wimbo huo.

 

“Pamoja na kuwajibu kuwa ndiyo mimi mwenye wimbo huo, bado jamaa hawakuridhika kabisa, wakaanza kuniuliza nilipo nikawaelezea baada ya kuelekea kama kuamini ndiyo mimi wakauliza tena kama nina nyimbo nyingine lakini kwa kuwa ukweli nilikuwa nazo niliwaambia ninazo kama arobaini hivi ila sijazitoa kwa maana ya kuzirekodi.

 

“Wale jamaa waliniuliza kama tunaweza kufanya biashara kwa pamoja kimuziki.

“Kutokana na mimi kuwa na shauku ya muda mrefu ya kupata mtu wa kunisaidia, hata sikujivunga, palepale niliwaambia sawa tunaweza kufanya.

 

“Wakanitumia nauli, nikaja Dar es Salaam ili tuonane, kusema kweli baada ya kufika niliwaona wako siriazi na walikuwa ni watu wenye maisha mazuri na biashara zao zilikuwa ziko safi sana.

 

“Basi baada ya kuwaona tukazungumza pale, kuna anaitwa Benny ambaye ni mfanyabiashara wa vitu vya umeme, simu na vitu vingine, tangu siku hiyo akanishika mkono na huyo ndiye aliyeanzisha rasmi kazi yangu ya muziki.

 

“Tukaanza kutafuta studio ili twende kurekodi, lakini kabla hatujaanza kuna mmoja kati yao akataka niwaimbie baadhi ya nyimbo zangu kati ya zile 40 nilizowatajia ili waweze kujiridhisha kabla ya kunipeleka studio.

 

“Nikaanza kwa kuwaimbia Wimbo wa Ritta, kisha Daima na Milele, pia nikaimba Wimbo wa Bado Umenuna, basi palepale wale jamaa wakakubali zaidi uwezo wangu.

 

“Baada ya kumaliza maelewano waliomba twende studio tukarudie Wimbo wa Bembeleza, maana waliona kama ulivyokuwa umerekodiwa kule Iringa na Tuddy, haukuwa vizuri sana.

 

“Tukaenda Studio za G2 na tukamkuta prodyuza Roy ambaye kwa sasa ni marehemu, alijaribu kuifanya lakini ile biti iliyokuwa imepigwa na Tuddy Thomas ilimshinda na kujikuta na yeye amepiga nyingine, hivyo ikawa kama haikupendeza, nikawaambia mabosi zangu naona kama haijakaa sawa, kama vipi tuachie tu ileile ya kwanza kwa maana ya ile iliyopigwa na Tuddy.”

 

Je, baada ya kuachia goma hiyo ya Bembeleza, je, maisha yake baada ya kurejea shule yalikuwaje na kwamba alikuwa akitarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza kidato cha sita?

USIKOSE JUMATATU IJAYO.

MUSA MATEJA | KILINGE | CHAMPIONI JUMATATU | 0715332033

Leave A Reply