The House of Favourite Newspapers

Mashabiki Simba, Yanga Watamba Wanakufa nyingi

0

MTAKULA nyingi! Unaweza kusema hivyo kutokana na namna makocha wa Yanga na Simba walivyozungumzia maandalizi yao kuelekea kwenye mchezo wa Dabi ya Kariakoo ambayo leo pale Uwanja wa Taifa, Dar mashabiki watajionea ‘live’.

 

Yanga yenye pointi 47 wakiwa nafasi ya tatu, inahitaji kushinda katika pambano hilo ili kupunguza idadi ya pointi za Simba wanaoongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na 68 wakifuatiwa na Azam FC wenye 48.

Bonge la mechi baina ya timu hizi kongwe ambapo zinakutana kwa mara ya pili kwenye Ligi Kuu Bara, mechi ya kwanza iliisha kwa sare ya mabao 2-2 na Simba walikuwa wenyeji safari hii Yanga ndiyo wenye mji wao.

 

Klabu hizi zinanolewa na makocha kutoka nchi moja, ndiyo ni Ubelgiji lakini kila mmoja ana falsafa yake kwenye ufundishaji soka. Makocha hawa wamejiunga wakati ligi zimeshaanza, Januari 9, 2020, Yanga ilimtangaza Kocha Luc Eymael kuchukua mikoba ya Mwinyi Zahera na mpaka sasa Mbelgiji huyo ameiongoza timu hiyo katika michezo 12 ya ligi kuu na miwili ya Kombe la FA.

Kwa upande wa Simba, wao Desemba 11, 2019 walimtambulisha Kocha Sven Ludwig Vandenbroeck kuchukua nafasi ya Patrick Aussems na mpaka sasa ameiongoza timu hiyo katika michezo 16 ya ligi na mitatu ya FA, na sasa wanakwenda kukutana kwa mara ya kwanza kesho.

 

Wakizungumza na Championi Jumamosi, makocha hawa kila mmoja alitamba ni lazima apeleke kilio kwa wapinzani wake huku wakifanya marekebisho kadhaa kabla ya mchezo huo.

 

Kocha wa Yanga, Eymael yeye amekiangalia kikosi chake na fasta akachukua maamuzi magumu ya kubadili ‘First Eleven’ atakayoitumia kwenye mchezo wake dhidi ya Simba.

 

Luc alisema mapema baada ya mchezo wao na Mbao ambao Yanga walishinda mabao 2-0, atafanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake ambacho kitacheza na Simba.

 

“Mashabiki wa Yanga waje kwa wingi kupata burudani kubwa katika dabi ambapo nitawachezesha wachezaji ambao hawakuwepo katika mchezo uliopita uliotukutanisha sisi na Simba, kwa upande wa kocha na benchi la ufundi hatuna hofu, presha ipo kwa mashabiki pekee,” alisema Luc.

 

Lakini kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, Luc amepanga kuwatumia mabeki watano kwa ajili ya kujilinda zaidi huku akimtumia Kelvin Yondani kucheza namba sita.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa wakati akimtumia Yondani kucheza namba sita, mabeki wa kati ni Mghana Lamine atakayecheza pacha na Juma Makapu huku mabeki wa kulia wakiwa ni Juma Abdul na Jafary Mohammed.

 

Alisema kuwa lengo la kuwatumuia mabeki watani nyuma ni kwa ajili ya kupunguza mashambulizi golini kwao yatakayoongozwa na Luis Miquissone, John Bocco, Meddie Kagere, Francis Kahata na Clatous Chama ambao ndiyo wachezaji tishio golini kwenye goli la Yanga.

 

Aliongeza kuwa katika safu ya kiungo inatarajiwa kuwepo mabadiliko kidogo tofauti na mchezo uliopita wa watani wa jadi, kwa kumuanzisha Feisal Salum ‘Fei Toto’ kucheza namba nane nafasi iliyochezwa na Mohammed Issa ‘Banka’.

 

Papy Tshishimbi anatarajiwa kucheza namba kumi iliyokuwa inachezwa na Mapinduzi Balama huku Haruna Niyonzima akicheza kiungo mshambuliaji anayetokea pembeni namba saba na Bernard Morrison kumi huku kumi akisimama Ditram Nchimbi.

 

“Kwa mujibu mazoezi yaliyofanyika juzi (Alhamisi) na leo (jana) Ijumaa huenda kikosi kikawa kina mabadiliko madogo kwa kuwaanzisha wachezaji ambao katika mchezo uliopita wa watani wa jadi hawakuwepo.

 

“Wachezaji watakaoingia katika kikosi hicho ni Fei Toto ambaye kocha ameonekana kumpa majukumu ya kucheza namba nane katika mazoezi yake na Makapu yeye atacheza namba nne nafasi iliyokuwa inachezwa Yondani ambaye yeye amebadilishiwa majukumu ya namba sita.

 

“Lengo ni kutowapa nafasi viungo wa Simba kucheza na kusogea kwenye goli letu kila mara ndiyo maana Yondani amepewa jukumu la kucheza namba sita atakayesaidiana na Fei Toto, Tshishimbi huku Morrison na Niyonzima wakiwa na kazi moja ya kumtengenezea nafasi za kufunga Nchimbi,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Kwa upande wa Sven, yeye amewaambia kweupe wapinzani wake, Yanga kwamba hata wafanyaje hawatoki kwenye mechi hiyo kutokana na kuhitaji matokeo mazuri mbele yao.

 

Mbelgiji huyo ameliambia Championi Jumamosi, kuwa wanataka kupata pointi za Yanga ambapo kwa maandalizi ambayo wamekuwa nayo wana uhakika mkubwa wa kuzichukua baada ya kuzikosa kwenye mechi iliyopita. “Kwanza tunajipongeza kwa sababu tulifanikiwa kuchukua pointi tatu tulipocheza na Azam ambayo ilikuwa mechi ngumu kwetu, baada ya kumaliza hiyo kwa sasa ni zamu ya kuchukua pointi kwenye mechi hii ya Jumapili.

 

“Tumekuwa na maandalizi mazuri tangu tulivyomaliza mechi yetu hiyo Azam na katika mechi hii na Yanga tunataka kupata pointi tatu kwa sababu tumekuwa na matokeo mazuri kwenye mechi za karibuni. “Ninachotaka ni kuona tunashinda mchezo huo na ili tuweze kushinda utaratibu wetu ni uleule wa siku zote wa timu kucheza zaidi eneo la mbele,” alisema Sven.

Leave A Reply