The House of Favourite Newspapers

Mambo 5 Kutikisa Uchaguzi 2020

0

DAR: Mbio za Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar 2020 zimezidi kushika kasi na kuwaacha wanasiasa matumbo joto kutokana na uchaguzi huo kuwa na mtikisiko wa kipekee. Gazeti la IJUMAA linachambua.

 

Mtikisiko huo unatokana na mgombea urais ajaye kuwa kitendawili kwa kuwa Rais wa sasa, Dk Ali Mohamed Shein anamaliza ngwe yake ya mwisho hivyo kutoa fursa ya uongozi mpya.

 

Uchaguzi huo ambao sasa unatazamwa kwa jicho la matamanio na pande zote za vyama vya siasa visiwani humo, unatajwa kuwa na mtikisiko mkubwa ikilinganishwa na uchaguzi mkuu wa Bara ambao Rais John Magufuli anatarajiwa kutetea nafasi yake kwa awamu ya pili.

 

MCHAKATO NDANI YA CCM, UPINZANI

Mchakato wa kumpata mgombea urais atakayesimamishwa na chama hicho, ni moja ya jambo kubwa linalotarajiwa kukitikisha CCM.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba tayari yapo makundi yaliyojiunga kuwaandaa watia nia wao.

 

Jambo hilo linawafanya wachambuzi wa masuala ya siasa kuamini kuwa kama CCM hakitakuwa imara kwenye mchakato mzima wa kumpata mrithi wa Dk Shein, basi upo uwezekano mkubwa wa CCM kugawaganyika kama ilivyokuwa kwa upande wa bara mwaka 2015.

 

Mgawanyiko huo unatazamiwa kuibuliwa na makundi ya makada wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ambao sasa wanatajwa makada maarufu wa chama hicho kutaka kuwania nafasi hiyo kama vile Dk Hussein Mwinyi, Shamsi Vuai Nahodha na Profesa Makame Mbarawa.

 

Upande wa upinzani Mshauri Mkuu wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad anatajwa kuendelea kuchanga karata zake.

Maalim Seif ambaye ni kinara wa upinzani visiwani humo, anatajwa kuwa na wakati mgumu kwa kuwa tayari amekihama Chama cha Wananchi (CUF) na kuelekea ACT Wazalendo.

Hali hiyo inatajwa kuwagawa Wazanzibar ambao ndiyo wanaona ni waasisi wa CUF tofauti na ACT-Wazalendo ambacho ni chama kichanga kisiasa.

 

WAZANZIBAR KUTAKA KUJIAMULIA

Suala la Wazanzibar kutaka kujiamulia mambo yao, ikiwamo kujichagulia mgombea wanayemtaka ni moja ya mambo ambayo yanatajwa kutikisa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

 

Hali hiyo inachagiza na chaguzi zilizopita ambazo mara kwa mara Wazanzibar wanadai kuchaguliwa mgombea urais na upande wa Bara. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wadadisi wa mambo visiwani humo wanadai kuwa, wanasiasa wakongwe Visiwani Zanzibar wanatajwa kusimama kidete ili kuhakikisha jambo hilo halijirudii.

 

Mmoja wa makada wanaotajwa ni Rais Mstaafu Amani Abeid Karume pamoja na Dk Mohamed Gharib Bilal, jambo ambalo linaleta mvutano wa kipekee hasa ikizingatiwa kuwa mgombea ajaye ni mpya.

 

KATIBA MPYA

Uhitaji wa Katiba mpya ni mojawapo ya mambo yanayotajwa kutikisa uchaguzi huo kama anavyofafanua Mbunge wa Malindi, Ali Saleh (CUF) alipozungumza na Gazeti la IJUMAA.

Alisema kuwa, Katiba mpya ni ngao ya utetezi wa maslahi mapana ya Zanzibar kutokana na kukithiri kwa migongano ya kiutendaji na malalamiko kutoka kwa Wazanzibar.

 

“Nilikuwa mjumbe wa Tume ya Jaji Warioba, Wazanzibar waliotaka Serikali tatu walikuwa zaidi ya asilimia 61, wakati bara walikuwa asilimia 63, kwa hiyo kusema Katiba mpya si jambo muhimu na limechacha kwa sasa ni sawa na kupotosha umma.

 

“Hili ni jambo ambalo litatikisa uchaguzi huu kwa sababu pia litatumika kama ajenda ya kuwashawishi wazanzibar walio wengi kumkubali mgombea urais atakayeteuliwa,” alisema.

 

KERO ZA MUUNGANO

Mbunge wa Welezo, Saada Mkuya (CCM) anasema suala la kero za muungano ni jambo lingine ambalo litatikisa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Alisema katika muono wa kawaida, Zanzibar imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo, lakini yapo mambo muhimu ambayo yanapaswa kutiliwa mkazi ili kutia chachu ya ukuaji wa uchumi wa visiwa hivyo kwa kasi zaidi.

 

“Iwapo kero za muungano zikitatuliwa ipasavyo zitaweza kuchachusha uchumi na kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa sababu yapo mambo ambayo tumekuwa tukiyazungumzia mara kwa mara kama vile suala la kodi ambapo bidhaa zinazotoka Zanzibar kuelekea Bara hutozwa kodi kubwa ilihali hizi ni nchi zilizoungana.

“Hili ni jambo ambalo wabunge tunapaswa kusimamia kwa sababu litaleta maendeleo kwa pande zote,” alisema.

 

AMANI

Suala la amani ni mojawapo ya mambo ambayo yanatajwa kutikisa katika uchaguzi mkuu hasa ikizingatiwa historia ya visiwani hivyo, inaonesha dhahiri kuwapo kwa visasi vinavyosababisha madhara kwa jamii ya Wazanzibar.

 

Baadhi ya wachambuzi wanatolea mfano mauaji yaliyotokea mauaji ya mwaka 2001 ambayo yalitokana na visasi vya kisiasa na kusababisha mtafaruki visiwani.

Hata hivyo, kulikuwapo na mwendelezo wa visasi ambavyo vilisababisha baadhi ya watu kumwagiwa tindikali, baadhi ya jamii kutoshirikiana jambo ambalo sasa linaonekana kuwa tishio.

 

Kutokana na hali hiyo, Mkuya ambaye pia ni waziri wa zamani wa fedha na uchumi anasema mtazamo wa kisiasa isiweke rehani amani iliyopo sasa visiwani humo.

“Amani iliyopo iendelee ili kueweza kuleta maendeleo zaidi. Wanasiasa tuna zile itikadi, tusivutane kwenye mitazamo ya kisiasa, ‘tu-focus’ katika ajenda kubwa ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema.

Stori: GABRIEL MUSHI, Ijumaa

Leave A Reply