The House of Favourite Newspapers

Mashabiki Yanga SC Waikataa ‘Sub’ Ya Kamusoko

KATIKA hali isiyotarajiwa, juzi Jumatano mashabiki wa Yanga walionyesha kukerwa na mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi la Yanga kwa kumtoa kiungo, Thabani Kamusoko na kumuingiza Raphael Daud wakati timu hiyo ilipokuwa ikipambana na Rayon Sports.

 

Tukio hilo lilitokea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar wakati wa mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika uliomalizika kwa suluhu ambapo katika benchi la Yanga, Noel Mwandila ndiye aliyekuwa kama kocha mkuu akisaidiana na Shadrack Nsajigwa.

 

Championi Ijumaa ambalo lilikuwepo uwanjani hapo likishuhudia mchezo huo, liliwasikia mashabiki wa Yanga wakipaza sauti za kukataa Kamusoko kufanyiwa mabadiliko dakika ya 66 na nafasi yake kuchukuliwa na Daud.

 

Mashabiki hao walitaka atolewe Juma Mahadhi au Geofrey Mwashiuya ambapo kwa mujibu wao, wachezaji hao walikuwa wameonyesha dalili za kuchoka, hivyo Kamusoko hakustahili kutolewa na badala yake angeendelea kuwepo uwanjani ili asaidiane na Daud.

 

Hata hivyo, mabadiliko hayo yalifanyika na ilipofika dakika ya 77, mashabiki hao wakaanza kuliimba jina la straika wao, Amissi Tambwe wakihitaji apewe nafasi ya kuingia uwanjani wakisema kwamba ndiye mkombozi wao baada ya kupona.

 

Kelele hizo zilizaa matunda dakika ya 84 ambapo Tambwe aliingia kuchukua nafasi ya Obrey Chirwa, mashabiki wakapongeza mabadiliko hayo.

 

Baada ya mchezo huo, gazeti hili lilimuuliza Mwandila juu ya sakata hilo ikiwemo kuzungumzia alivyoona viwango vya wachezaji hao ambao wamerejea uwanjani hivi karibuni.

 

“Nadhani kwa sasa si suala la kuzungumzia kiwango cha mchezaji mmojammoja, Kamusoko kama mnavyojua hivi karibuni amerejea kutoka kwenye majeraha na amekuwa akifanya vizuri.

“Tambwe yeye tumempa muda mfupi sababu na yeye hayupo fiti kwa asilimia zote, kwa hiyo huwezi kumuongelea uwezo wake, ningependa watu wazungumzie kiwango cha timu kwa jumla na siyo mtu mmojammoja,” alisema Mwandila.

Comments are closed.