Mfu Aliyerudiwa na Uhai-12

 ILIPOISHIA WIKIENDA

Shangazi aliporudi tena chumbani na kuniona nilivyokuwa akaniambia:

“Nimeshampigia mama yako, amesema atafika muda si mrefu lakini kutokana na hali yako ilivyo, hatutamsubiri. Naita teksi twende hospitali.”

Dakika chache tu baadaye nikawa kwenye teksi nikipelekwa hospitali. Maumivu yalikuwa makali. Nilikuwa siwezi hata kukaa kwenye kiti.

Ilitokea bahati nilipofikishwa tu hospitali nikajifungua; yaani kama teksi ingechelewa kidogo tu ningejifungulia ndani ya teksi.

Nilijifungua mtoto wa kike. Nikashukuru Mungu. Kwangu mimi yeyote alikuwa mtoto awe wa kike au wa kiume.

Masaa mawili baadaye mama alifika hospitali kuniona. Ni kwamba alipofika nyumbani Kigamboni aliwasiliana na shangazi akamwambia tupo hospitali na nimeshajifungua tayari.

SASA ENDELEA…

MAMA alifurahi kusikia nimezaa kwa usalama. Niliona uso wake ulikuwa na tabasamu wakati wote.

Wakati anafika nilikuwa namnyonyesha mwanangu. Mwenzenu nimeshakuwa mama. Kitoto kizuri chenye afya. Sura ilikuwa kama ya baba yake lakini mashavu na paji la uso ni kama mama yake.

Nilifurahi kuona mwanangu alikuwa amechukua pande zote mbili. Alikuwa ameshabihiana na baba yake na pia mimi mama yake.

Nilifahamu Macheo atafurahi atakapomuona.

“Maziwa yanatoka vizuri?” mama akaniuliza.

“Yanatoka.”

“Basi endelea tu kumnyonyesha.”

“Maziwa yenyewe yanayotoka machafu.”

“Yana nini?”

“Mazito kama mtindi halafu yana rangi mbaya, siyo meupe.”

“Hebu yachomoe midomoni uyakamue niyaone.”

Nikalichomoa titi lililokuwa midomoni mwa mwanangu na kulikamua. Matone ya mziwa mazito yakatoka.

“Si unayaona?”

“Maziwa ya kwanza ndivyo yalivyo, hayakuharibika. Hayo ndiyo yanayotakiwa umnyonyeshe mtoto mara tu unapojifungua. Yana protini nyingi.”

“Mmh…nilitaka kuyakamulia pembeni. Nilidhani ni machafu.”

Mama akacheka kisha akamtazama shangazi.

“Zamani baadhi ya kina mama walikuwa wakiyakamua na kuyamwaga mpaka yatoke maziwa meupe,” akamwambia.

“Mpaka sasa wapo. Wanasema ni machafu ukimnyonyesha mtoto ataharisha.”

“Ni kukosa kufahamu tu lakini haya maziwa ni bora sana na yapo mwanzo mwanzo tu baadaye hutayaona tena.”

“Ndiyo yanatoka mwanzo mwanzo tu. Baadaye yanatoka yale ya kawaida, sasa kama uliyakamulia pembeni ndiyo umeshamkosesha mwanao protini muhimu. Mwisho unasema amerogwa.”

Nikawa nimepata funzo. Kama mama asingeniuliza nisingefahamu yale maziwa ya mwanzo yana maana gani. Kweli kuna mengi ambayo tunatakiwa kuyafahamu kuhusu ulezi wa watoto wetu.

“Baba ana habari kuwa nimeshazaa?” nikamuuliza mama.

“Anayo habari. Shangazi yako ametupigia kutufahamisha.

“Lakini naona hatafika.

“Miguu bado inamsumbua.”

“Kwani unadhani utakaa hapa hadi lini, usishangae hata sasa hivi ukapewa ruhusa,” shangazi akaniambia.

Nikataka kusema Macheo hana habari kuwa nimezaa lakini nikaogopa. Ningeonekana nampenda sana Macheo. Nikanyamaza.

Kama alivyosema shangazi baada ya daktari kuhakikisha kuwa nilikuwa salama mimi na mwanangu, akaniruhusu nirudi nyumbani.

Tangu nilipokuwa na mimba hadi nilipozaa ilikuwa siri. Si watu wengi waliofahamu kama nilikuwa na mimba zaidi ya watu wa familia yetu na hivyo hata nilivyozaa waliofahamu walikuwa ni wanafamilia tu.

Kwa sababu hiyo sikupata wageni wengi walionitembelea kunipa hongera.

“Mama, mtoto wangu ataitwa nani, mbona hamsemi?” nikamuuliza mama tulipofika nyumbani.

Kabla ya mama kusema chochote nikasema:

“Au mpaka Macheo afike?”

“Hata kama atafika. Kwani alipokupa mimba ulikuwa mke wake? Alikuwa amekuoa?” Mama akaniuliza kwa ukali kidogo.

“Kama hakuwa amenioa?”

“Hawezi kumuita mtoto atakavyotaka yeye. Asubiri mtoto mwingine atakayemzaa ndani ya ndoa.”

“Sasa huyu ataitwa nani?”

“Huyo ni Mayasa.”

Mama yangu naye anaitwa Mayasa.

“Nimekuzaa wewe mama’angu,” nikamwambia mama.

“Mayasa Macheo…Mayasa Macheo…!” nikawa namuita yule mtoto.

Nikachukua simu yangu na kumpigia Macheo. Nikamfahamisha kuwa nimeshazaa mtoto wa kike.

“Hongera,” akaniambia kwenye simu.

“Nimemzaa mama yangu.”

“Ni heri. Nitafika huko muda si mrefu.”

“Macheo amesema atafika,” nikamwambia mama baada ya kukata simu.

“Na afike amuone mwanawe.”

Baada ya kuzaa yule mtoto ndipo nilipofahamu umuhimu mwingine wa kuwa na mama. Mama ndiye aliyenisaidia kila kitu kumhudumia mtoto. Alinifunza namna bora ya kumnyonyesha, kumuogesha na mambo mengine.

Mimi nilikuwa namnyonyesha tu lakini kila kitu alikuwa akifanya mama, utadhani yeye ndiye aliyezaa.

Nikawaza kama nisingekuwa na mama yangu, nani angenisaidia? Mama ni muhimu sana.

Baada ya masaa mawili hivi, Macheo akafika nyumbani. Aliingizwa chumbani na shangazi. Mama na wifi yake wakatoka mle chumbani na kutuacha.

Macheo alipoingia humo chumbani alikuwa amefadhaika lakini alipomuona mwanawe, tabasamu pana likachanua kwenye uso wake. Kweli mtoto baraka na ni heri.

Nilimpa mtoto amshike, akamshika huku akiendelea kutabasamu.

Kwa vile Macheo alikuwa akifahamu kuwa mama yangu anaitwa Mayasa na nilishamwambia nimemzaa mama. Akawa anamuita mtoto.

“We bi mkubwa…Mayasa… sura kama mama yako…”

“Mh… amefanana na wewe huyo…” nikamwambia.

“We unaona pua ile na macho…wewe mtupu.”

“Mh…kafanana na wewe bwana. Huoni hili komo hapa na hiki kidevu”

“Sura ya mtoto inabadilikabadilika. Leo utasema kafanana na mimi, kesho utaona kafanana na wewe.”

“Kwani ni kinyonga?”

“Si kinyonga, ndivyo watoto walivyo. Subiri ipite wiki utaona.”

“Mh…Baba Mayasa wadanganya….”

Nilipomuita baba Mayasa Macheo alifurahi.

Mtoto akaanza kulia.

“Hebu mnyonyeshe, naona analia.”

“Ni mlizi tu, muda wote alikuwa ananyonya.”

Nikamchukua yule mtoto na kumpa ziwa, akawa ananyonya.

“Unaona amenyamaza.”

“Anataka akae kwenye ziwa muda wote.”

“Ukiona hivyo ufahamu kuwa hata wewe ulikuwa hivyohivyo. Ulikuwa hubanduki kwenye ziwa.”

Macheo aliponiambia hivyo; tukacheka.

“Baba Mayasa yote tisa, unipe kama laki mbili hivi nimrudishie shangazi pesa zake za hospitali na mimi nipate za kutumia na mtoto.”

“Chukua elfu hamsini. Kesho nitakupatia nyingine.”

Macheo alitia mkono mfukoni akatoa shilingi elfu hamsini na kunipa.

“Kesho utafika saa ngapi?” nikamuuliza.

“Muda kama wa leo.”

“Sawa.”

Tuliendelea kuzungumza kwa karibu saa nzima kabla ya Macheo kuaga na kuondoka. Macheo aliendelea kufika nyumbani karibu kila siku. Na mama yangu aliendelea kubaki hapo nyumbani kunisaidia.

Siku ya arobaini ya mtoto tulisoma maulidi. Baada ya miezi miwili kupita nikiwa kulekule Kigamboni ndipo tulipoanza tena mipango ya harusi. Macheo akaniambia amepanga kwenda kuishi na mimi mkoani kwao.

“Wapi?”

“Tanga.”

“Kwa nini?”

“Nina wasiwasi na yule mchumba wako wa kwanza. Mara kwa mara anapita na gari yake mbele ya nyumba yangu Tabata.”

“Anafika kule?”

“Anafika. Nahisi kama anakutafuta wewe au kukuchunguza. Anahisi uko kwangu. Kwa hiyo nimeamua kuomba uhamisho kazini twende Tanga. Yule mzee anaweza kutuletea matatizo kwa sababu naona kama ana chuki.”

“Ni sawa kubadili hali ya hewa lakini tutaoana hapahapa.” “Tutafunga ndoa hapahapa. Baada ya ndoa ndiyo tutaondoka. Nadhani uhamisho wangu unaweza kuwa tayari.


Loading...

Toa comment