The House of Favourite Newspapers

Mashehe wa Uamsho Washinda Rufaa

0

VIONGOZI wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheik Farid Hadi Ahmed na wenzake 35 wanaokabiliwa kesi ya ugaidi wameigaragaza tena serikali mahakamani, baada ya kushinda rufaa ya Serikali iliyokuwa ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuwafutia mashtaka 14 kati ya 25 yaliyokuwa yakiwakabili.

 

Hatua hiyo inatokana na hukumu ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa ya Serikali ikisema kuwa mamlaka ya DPP kukata rufaa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu na mahakama za chini zenye mamlaka ya ziada kutekeleza mamlaka yake una mipaka isipokuwa kwa kupinga adhabu au washtakiwa kuachiwa huru.

 

Aprili 23, 2021, Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka 14 baada ya kukubaliana na hoja za mawakili wao, Daimu Halfani, Juma Nassoro, Jeremiah Mtobesya na Abubakar Salum, kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka hayo kwa kuwa makosa wanayotuhumiwa yanadaiwa kutendeka Zanzibar.

 

Serikali kupitia kwa DPP ilikata rufaa Mahakama ya Rufani kuupinga lakini wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo mawakili wa washtakiwa hao waiibua pingamizi dhidi ya rufaa hiyo ya Serikali.

 

Pamoja na mambo mengine walikuwa wakidai kuwa DPP hana mamlaka tena ya kukata rufaa chini ya kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Rufani.

 

Walidai kuwa kifungu hicho kilishaondolewa na Mahakama ilipotamka kuwa kinakinzana na Ibara ya 13 (1) na (2) na ya 6(a) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kesi namba 27 la mwaka 2018, Joseph Steven Gwaza dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 

Akijibu pingamizi hilo, DPP alidai kuwa uamuzi huo wa mahakama katika kesi hiyo ya Gwaza ulihusu uamuzi mdogo usiomaliza shauri (interlocutory orders) na kwamba uamuzi huo unaopingwa wa kuwaondolewa mashtaka hayo unahitimisha mashtaka hayo ya jinai.

 

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika hukumu yake iliyotolewa jana jopo la majaji watatu walioisikiliza rufaa hiyo lililoongozwa na Jaji Stella Mugasha, akishirikiana na Shaban Lila na Winfrida Korosso, ilikubaliana na hoja za pingamizi la mawakili wa Uamsho na kuitupilia mbali rufaa hiyo ya Serikali.

 

Leave A Reply