The House of Favourite Newspapers

Maskini familia hii! Ukisikia mateso yao, lazima utoe machozi

UKISIKIA mtihani mkubwa kwenye maisha ndiyo huu! Maskini, familia ya Mzee Lenati Semgweno ya Kijiji cha Makuyu wilayani Mvomero, Morogoro imepita na inapita kwenye mateso makali ambayo ukiyasikia, lazima machozi yakutoke.

Mzee huyo anasema amepita kwenye mitihani mingi baada ya kuzaa watoto wanne walemavu na mmoja akiwa ni mjukuu ambaye ni watano.

 

Gazeti la Ijumaa limemtembelea mzee Semgweno na kuzungumza naye juu ya wanaye hao.

Semgweno anasema mtoto wake wa kwanza alimzaa mwaka 1990 akiwa mwenye afya njema kabisa, lakini wakati akiwa mdogo alianza kuumwa homa kali kama ya degedege iliyomfanya alegee viungo vyote.

Anasema pamoja na hali hiyo, lakini mtoto huyo aliendelea kukua na kuanza kutembea ila alipofikisha umri wa miaka 10 ilikuwa ndiyo mwisho wa kukua na kushindwa kuinuka.

 

Mzee huyo anasema hali hiyo ndiyo iliyowapata watoto wake wengine waliofuata na hata mjukuu wake.

Anasema kinachomuumiza mtoto wake wa pili ambaye anaitwa Evarist aliyemzaa mwaka 1993 naye alikuwa na tatizo hilohilo kama la kaka yake na kila wanapofikisha umri wa miaka 10, basi hawezi tena kutembea.

 

“Unajua unapozaa na kukutana na mtihani kama huo, unajipa moyo na kumshukuru Mungu kuwa, utazaa mtoto mwingine mwenye afya huku ukiendelea kulea yule mwenye matatizo, lakini kwa bahati mbaya, unapata tena mwenye shida hiyohiyo,” anasema baba huyo.

Semgweno anaendelea kusema kuwa kinachomshangaza zaidi ni kwamba yeye na mkewe walipopanga kuzaa tena mtoto wa tatu mwaka 1997 ambaye ni wa kike aitwaye Vaileth naye alipata tatizo kama hilo.

Alisema amekuwa akiwapeleka hospitali mbalimbali, lakini hakuna msaada waliopata zaidi tu ya dawa za maumivu.

 

“Sitaki kukuelezea uchungu tunaopata kwa watoto hawa, kwa kweli inauma sana mpaka watu wameanza kutupa majina ya ajabu na kutunyanyapaa kabisa kuhusiana na watoto wetu hasa pale tulipozaa mtoto wa nne, Emanuel mwaka 2000 naye akawa na tatizo hilohilo na mjukuu wangu ambaye mtoto wetu wa kwanza hakukumbwa na tatizo hilo,” anasema.

 

Anasema kuwa maisha yao yanazidi kuwa magumu siku hadi siku kwa sababu wakila mlo mmoja jioni ni mpaka jioni ya siku inayofuata huku kukiwa na uhaba mkubwa wa maji maana watoto hao wanajisidia kila kitu wakiwa wamekaa.

 

“Mimi unavyoniona baba yao hapa ni mzee sasa, sina nguvu kabisa, mama yao ndiye huyo, hata shamba inashindikana kwenda kwa sababu hawa watoto mtu mmoja au wawili kuwaangalia ni ngumu sana. Maji yenyewe tunafuata mbali sana kiasi cha mwendo wa nusu saa na hapa ili maji yatoshe yanahitaji pipa nne,” anasema baba huyo.

 

Baba huyo anaongeza kuwa wanahitaji sana msaada wa kuchimbiwa kisima ambacho kingeweza kuwasaidia kuondokana na tatizo la maji, angalau watoto hao waoge hata mara mbili kwa siku na angalau kupata chakula cha kuwapa.

 

“Tumekuwa wanyonge siku zote kutokana na taabu wanazopata watoto wetu. Sisi tumekuwa wazazi wa simanzi, lakini kamwe hatutaacha kumshukuru Mungu kwa ajili ya watoto wetu.

“Kama una chochote cha kutusaidia mimi familia yangu unaweza kutumia namba ya mtoto wetu, Elizabeth namba 0717 502 178,” anamalizia mzee Semgeno.

Stori: NEEMA ADRIAN, DAR

Comments are closed.