The House of Favourite Newspapers

Masogange Sasa Chunga Sana Nyendo Zako!

Agness Gerald.

KWAKO mrembo uliyechipukia kwenye kilinge cha u-video queen, Agness Gerald almaarufu Masogange. Mambo vipi? Habari za siku? Kitambo kidogo sijakutia machoni. Maisha haya nayo yanatufanya tusionane siku hizi.

Kipindi fulani niliwahi kukutembelea nyumbani kwako mapema mwaka huu, lakini kwa bahati mbaya nilishindwa kukuona. Niliambiwa na mfanyakazi wako wa ndani umetoka. Kutokana na ubize wa majukumu yangu, nikiri tu hatujaonana muda mrefu.

 

Yawezekana tungekuwa tunaonana mara kwa mara, pengine ningekueleza ninachotaka kukueleza tukiwa laivu. Lakini kwa sababu ya ubize wa kazi, ninalazimika kukuandikia barua hii nikiamini utaisoma na kufanyia kazi ushauri wangu.

Masogange dhumuni la mimi kukuandikia barua hii leo ni kutaka kukueleza kwamba kwa jinsi mwenendo wako unavyokwenda, yakupasa ujitathimini na kujichukulia hatua mustakabali wa maisha yako.

 

Nimekufuatilia tangu kipindi kile ulipokamatwa nchini Afrika Kusini kwa msala wa madawa ya kulevya. Hata hivyo, baadaye ilibainika kwamba hayakuwa madawa ya kulevya. Kama muungwana nilikuelewa, hilo likapita na tukaendelea na maisha.

Hilo lilipomalizika, baadaye wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokuwa anataja orodha yake ya watuhumiwa wa madawa ya kulevya, nilishtuka tena kusikia nawe umeingizwa kwenye orodha hiyo.

 

Kesi ikaunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mahakama ikakukuta na hatia ya matumizi ya madawa ya kulevya. Hapo ndipo ninapoliona tatizo. Rafiki yangu, kwa kuwa kweli imethibitika unatumia madawa ya kulevya, yakupasa sasa kuwa makini sana.

Wewe ni mrembo, haipendezi kutopea kwenye matumizi ya

madawa ya kulevya. Kama starehe zipo nyingi, lakini ya madawa ni vyema ukaiogopa kama ukoma. Madawa ya kulevya huwa hayajawahi kumuacha mtu salama.

 

Mifano ipo wazi, wala haihitaji kukuelezea sana ili unielewe, jifunze tu kupitia dada yako, mwanamuziki wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’. Ulimuona jinsi alivyopata tabu katika suala zima la kujinasua kwenye madawa ya kulevya.

Unajua kilichotokea kwa kaka yako, msanii wa Bongo Fleva, Rashid Makwiro ‘Chid Benz’. Tulipoteza hazina ya taifa. Nani ambaye alikuwa haguswi na muziki wa Chid Benz? Wangapi walikuwa wanavutiwa na ile sauti yake ya mamlaka?

Baada ya kutopea kwenye madawa ya kulevya, biashara yake imeishia hapo. Anajitahidi kujinasua, lakini inashindikana. Ameshakwenda soba mara kadhaa, lakini matokeo yamekuwa hafifu. Tunampoteza Chid Benz huku tunamuona.

 

Masogange una jina kubwa kwenye tasnia ya burudani nchini. Unaweza kufanya makubwa kama utaamua kujishughulisha na kukaa mbali kabisa na viashiria vya madawa ya kulevya. Madhara ya madawa ya kulevya ni makubwa, kama umeonekana umeanza, basi ni wakati wako kuacha.

Kama unaona tatizo hilo limeshafika kwenye hatua ya juu na unashindwa kuacha, ni wakti huu wa kuwaona wataalam wa kukushauri au kwenda soba kufundishwa namna bora ya kuacha kabisa utumiaji wa madawa ya kulevya.

 

Amua kweli kuacha, moyo wako uwe na dhamira ya kuacha hapo ndipo utakapoweza kuacha kabisa madawa ya kulevya. Moyo ukiwa haujaamua, hata ukienda soba bado itakuwa ni kazi bure.

Mimi nikutakie kila lakheri katika maisha mapya utakayokwenda kuyaanza kwani ninaamini utakwenda kuacha kabisa. Ukiendelea, jiandae kuwa kama Chid Benz.

Ni mimi kaka yako;

Comments are closed.