The House of Favourite Newspapers

MASTAA BONGO; UMRI UNAKWENDA, WANARUDI KUISHI KITOTO

Irene Uwoya

KWETU akiwepo mtu mwenye umri mkubwa halafu akawa anazungumza na kufanya mambo ya vijana, malipo yake ya kwanza huwa ni KUDHARAULIKA, baadaye jina la ‘Mzee Kijana’ humfuata nyuma.

Nadra sana kwa Mzee Kijana kupata hata salamu na heshima stahiki mbele ya jamii. Siyo hilo tu, hata kuwa mjumbe wa nyumba kumi kwake ni kazi ngumu.

Mzee Kijana hubaki kuwa kichekesho tu, akifika mahali ataongea atawafurahisha watu kwa simulizi zake za ‘mzee unanikokea moto; unataka kuninyima nini?’ Basi kazi yake inakuwa imeishia hapo.

Ukiangalia ulimwengu wa mastaa wetu wa Kibongo umejaa pomoni ‘Wazee Vijana’; unajiuliza mwisho wao utakuwa nini, ndiyo wawe vichekesho tu na maisha yao yakomee hapo? Unajikuta unasema HAPANA!

Kazi ya uandishi ni pamoja na kuonya na kufundisha; vipi makala haya isizifanye kuwasaidia baadhi ya mastaa wetu ‘Wazee Vijana’ kuweza kutambua thamani yao na kusudi jema lililowaleta duniani?

Bahati nzuri wengi kati ya wasanii wa Kibongo wamepita kwenye mikono ya UWAZI, wakasaidiwa kukuza vipaji vyao na kuweza kwa namna fulani kujinasua na mkwamo wa kimaisha; tunawajua walikotoka na walipo.

Natolea mfano msanii kama Irene Uwoya, Wema Sepetu, Aunt Ezekiel, Afande Sele, Diamond na wengine wengi miaka ya nyuma ya ujana wao walikuwa hawakosi vituko, walijaa mauzauza; kwa wakati ule haikuwa SO!

Lakini leo ulimwengu umebadilika; kiki za picha za utupu, video za ngono na ujanja wa kuvuta bangi na unga haziwalipi wasanii, zinawafedhehesha na kuwaondolea thamani ya ustaa wao.

Kwa msingi huo unapomuona Irene Uwoya leo anaweka picha ya msisimko wa kingono inayoonyesha kiwango kikubwa cha mwili wake wakati ni mke na mama wa mtoto na kusikia eti Wema anatuhumiwa kuvuta bangi, kwa umri wake ulivyo! Hupati shida kuwaita wasanii wa aina hiyo ni Wazee Vijana.

‘Wazee Vijana’ thamani yao ni ndogo sana kwenye jamii, hubaki kuwa wafurahisha watu. Mzee Kijana kutongozwatongozwa ovyo, kutaniwa hata na watoto ndiyo maisha yake hana kazi nyingine kubwa.

Je, tuwaache baadhi ya mastaa wetu waishi maisha haya? NO!

Hakuna namna mastaa wetu wanatakiwa kubadilika. Gari hutembelea gia kulingana na hali ya barabara, penye mlima hatumtarajii dereva kutumia gia nyepesi kuupanda.

Umri nao kadhalika, kwa msanii mwenye umri mkubwa hatakiwi kuishi maisha ya kitoto labda awe kaamua kuwa kichekesho kama Mzee Kijana.

Ndiyo maana hivi karibuni Uwoya alipoamua kuyarudia ya utotoni mwake kwa kupiga picha za aibu alipata tabu sana, alishambuliwa kwenye mitandao ya kijamii mpaka nikatamani kumuombea msamaha.

Ni kweli ujana una mambo mengi, lakini unapokuwa mtu mzima wewe ndiyo mama, ndiyo baba lazima ukubali kuyaacha maisha ya ujana ili ujenge maisha yako mema ya baadaye vinginevyo utatangatanga na maisha ya kihunihuni mpaka makunyanzi yatakapofunika macho na mfukoni hautakuwa na kitu cha kujivunia.

Kuiga mema si jambo baya; tuwaige walioacha Uzee Kijana wakakamata fursa maisha yao yanakwenda vyema. Jacqueline Ntuyabaliwe alikuwa

Miss Tanzania 2000 akawa mwanamuziki, akaishi kisanii kwa muda mfupi, alipoona amekuwa mtu mzima akayaweka kando maisha hayo akakamata fursa na sasa ni mke wa Mzee Reginald Mengi, anajenga maisha bora ya familia yake.

Hoyce Temu, alikuwa Miss Tanzania 1999, sina shaka mambo ya ujana aliyafanya baada ya kupata umaarufu, lakini naye alipoona amekuwa akasema ‘Uzee Kijana; NO! akajipanga sasa ni mjasiriamali.

Hawa ni kwa uchache tu, wapo wasanii wengi waliotambua kuwa wamekua wakaachana na ujana wakafanya vitu vya maendeleo na leo ni msaada kwa taifa na familia zao. NINYI wa ‘usinizeeshe’ endeleeni kukaa utupu na ‘kula bata’ ila mjue MTAPATA TABU SANA.

MAKALA: MWANDISHI WETU, UWAZI

Comments are closed.