The House of Favourite Newspapers

Mastaa Hawa Wamepita Na Upepo Wa Diamond Na King Kiba Yumo Mr Blue, Chid Benz

0
Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz.

DIAMOND Platnumz na King Kiba; ni vinara wa muziki nchini Tanzania ambao wameweka utimu wenye lengo la ushindani kwenye muziki wao, lakini imekuwa ni ngumu kwa wasanii wenzao na watayarishaji kufanya kazi na wakubwa hao kwa wakati mmoja.

 

Ushindani huo unawalazimisha wasanii na watayarishaji wa muziki kuchagua upande.

Kama umechagua upande wa King Kiba, basi ni wazi upande wa Diamond au Mondi ni ngumu kupata nafasi, maana tayari umejipambanua kuwa upo katika timu gani.

 

Hata hivyo, kuna wasanii na watayarishaji muziki Bongo wamefanikiwa kuepuka mtego huo, ingawa ni kipindi cha nyuma ambapo upinzani wa wawili hao ulikuwa haujaota mizizi kama ilivyo sasa.

Msanii wa Bongo Fleva, Alikiba  ‘King Kiba’.

CHID BENZ

Miongoni mwao ni msanii mkongwe wa Hip Hop Bongo, Chid Benz ambaye miaka ya nyuma alikuwa akishirikishwa mno na wasanii wenzake kutokana na sauti yake ilikuwa inauzika kwa urahisi na kufanya wimbo husika kupendwa na wengi.

 

King Kiba alimshirikisha Chid Benz katika ngoma yake ya Far Away ambayo ilifanya nab ado inafanya vizuri huku Diamond akimpa shavu katika ngoma yake ya Nalia na Mengi. Hata hivyo, wawili hao hawakufanya video ya ngoma hiyo.

 

MR BLUE

Mwingine ni Mr Blue ambaye ana ukaribu mno na wakali hao wawili. Baada ya Diamond kujiita Simba; jina alilokuwa analitumia Mr Blue aliamua kujipa jina la Nyani Mzee ili kuondoa tetesi zilizokuwa zinashika kasi kuwa hilo litaleta bifu kati yao baadaye, lakini hilo halikutokea.

Staa wa muziki wa Bongo Fleva Kheri Sameer ambaye wengi tumemzoea kwa jina la Mr Blue.

Diamond alimpa shavu Mr Blue kwenye ngoma yake ya ya Nakupa Moyo Wangu. Pia walikuja kukutana tena kwenye ngoma ya marehemu Ngwea ya BBM ambayo Chibu aliimba kiitikio.

Mr Blue akaja kumshirikisha King Kiba kwenye ngoma yake ya Mboga Saba baada ya kutokea kwenye video ya ngoma yake nyingine ya Pesa.

 

QUEEN DARLEEN

Mwanamama Queen Darleen naye ni miongoni mwa waliofanikiwa kupita na upepo wa wakali hao wa Bongo Fleva. Aliinasa sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa Kings Music kwenye ngoma yake ya Wajua. Darleen anasema; “Sijawahi kuona prodyuza labda wa King Kiba akifanya kazi kwa Diamond na prodyuza wa Diamond akifanya kazi na King

 

Kiba, kweli sijaona. Nafikiri hawajapata nafasi ya wao wenyewe kupangilia hilo, lakini msanii mmoja kati yao akitaka kufanya kazi na prodyuza yeyote sidhani kama atakataka, akikataa nadhani atakuwa hayupo sawa,” anasisitiza Queen Darleen.

 

Queen Darleen aliwahi kufanya ngoma mbili na Diamond za Zilipendwa ambayo ilipendwa mno na vijana kwa kuwa unawakumbusha mbali na ngoma nyingine ya Quarantine.

 

MOCCO GENIUS

Mtayarishaji wa muziki Bongo, Mocco Genius kutoka Studio za Imagination Sound, alianza na King Kiba kwa kumtengenezea ngoma iitwayo Mshumaa, akaja kutengeneza ngoma yake nyingine ya Cheche akiwa na msanii wake, Zuchu.

 

Mtayarishaji Mocco anasema watu wanaogopa kufanya kazi na mastaa hao bila sababu za msingi, lakini anachojua wenyewe hawana neno.

 

“Watayarishaji wana hofu tu kwa sababu suala la prodyuza kufanya kazi na wasanii tofautitofauti ndilo jukumu lake la msingi,” anasema Mocco.

 

NAVY KENZO

Kundi la Navy Kenzo linaloundwa na Nahreel na Aika; hawa ndiyo wamefanikiwa kupitia vizuri zaidi katikati ya zile timu za Mondi na King Kiba.

Nahreel ndiye aliyetengeneza ngoma ya Diamond ya Nana iliyotoka mwaka 2015. Mwaka 2017, Navy Kenzo wakamshirikisha King Kiba kwenye ngoma yao iitwayo Lin. Mwaka 2018 wakampa shavu Diamond kwenye ngoma yao ya Katika huku Nahreel akisimama tena kama prodyuza.

 

MARCO CHALI

Mtayarishaji wa muziki Bongo, Marco Chali anayefanya shughuli zake katika Studio za MJ Records Records, amefanya kazi na vijana hao wa Kariakoo akitengeneza Ngoma ya King Kiba ya Mapenzi Yana-run Dunia’ na baada ya miaka kadhaa akasuka Ngoma ya Kesho ya Diamond.

 

KIGOMA ALL STARS

Pamoja na uhasimu wao unaotokana na ushindani wa kimuziki, wawili hao waliwahi kusikika katika ngoma moja ya Kigoma All Stars ‘Nyumbani’ baada ya King Kiba kukosekana kwenye ngoma ya kwanza ya mradi huo.

 

STAREHE GHARAMA

Pia Diamond na King Kiba walitokea wakiwa wameketi sehemu moja kwenye video ya Ngoma ya Tundaman iitwayo Starehe Gharama.

MAKALA; ELVAN STAMBULI, BONGO

Leave A Reply