MASTAA HUKU NI KUCHEZEANA AKILI

MAHUSIANO ya kimapenzi yanachukua nafasi kubwa sana kwenye maisha ya binadamu. Hapa nawazungumzia wale ambao ni watu wazima, wenye akili zao timamu na wanajua maana ya kuwa na mtu, namaanisha mpenzi.  

 

Uhusiano wa kimapenzi ni kitu siriasi sana na ndiyo maana wanasaikolojia wanasema kwamba, ili uwe na amani katika maisha yako, unatakiwa kuwa makini sana katika kumchagua mtu atakayekuwa ubavu wako. Ukikosea kidogo tu, maisha yako lazima yatakuwa na mushkeli.

 

Ndiyo maana tunasikia kuna watu wameamua kunywa sumu na wengine kujinyonga kwa sababu ya kuvurugwa na wapenzi wao. Wengine wanafikia hatua ya kuchanganyikiwa na kushindwa kutimiza majukumu yao kwa sababu wapenzi wao wamewatendea ndivyo sivyo.

 

Hii yote inaonesha kuwa mapenzi ni sekta nyeti katika maisha ya binadamu. Lakini wakati ukweli ukiwa hivyo, wapo watu wanachukulia mapenzi kama kitu cha mzahamzaha. Hawako makini kabisa kwenye suala hilo. Baadhi wamekuwa wakibadili wapenzi kila kukicha, yaani kwao ni fasheni. Wapo ambao wanadiriki kuingia kwenye ndoa na kutoka, wanaona ni jambo la kawaida tu. Hawa ndiyo wale watu tunaosema hawako siriasi na maisha yao.

 

Wakati hali ikiwa hivyo, wapo mastaa ambao niseme tu kwamba wanatuchezea akili zetu kupitia sekta hii ya mapenzi. Katika kuwasilisha kile ninachotaka kukifikisha kwako, nirejee ndoa ya staa wa filamu Bongo, Irene Uwoya aliyofunga na mwanamuziki Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’.

Wakati taarifa za wawili hao kufunga ndoa ya Kiislam baada ya Uwoya kubadili dini zikisambaa, mimi nilikuwa mtu wa kwanza kupinga kwamba hakukuwa na ndoa. Nilisema hayo kwa sababu mbili za msingi; kwanza Irene na Dogo Janja wanapishana kiumri kwa kiasi kikubwa. Vijana wa mjini wanasema kuwa, Irene kuwa mke wa Dogo Janja ni ‘kumbemenda’.

 

Achilia mbali hilo la umri ambalo baadhi wanasema wala siyo ishu, namna ndoa hiyo ilivyofungwa kulikuwa na vingi viulizo. Ilifungwa kwa siri sana na mbaya zaidi baadhi ya watu waliohudhuria walipoulizwa kama ni ndoa kweli au kiki, walisema ni kiki kwa sababu kulikuwa na filamu wamecheza ikionesha Uwoya anaolewa na Dogo Janja.

 

Licha ya watu kusema ilikuwa ni kiki, wenyewe walisisitiza kwamba wameoana na kweli wakawa wanaishi pamoja kule Makongo Juu jijini Dar kama mke na mume. Mimi nikasema tena kwamba, hakuna ndoa na nikafafanua kuwa, kitakachofuata baada ya siku chache baadaye ni wawili hao kuachana kwa kuwa ndoa ya Kiislam inaruhusu. Na hapo tayari watakuwa wameshapata umaarufu zaidi.

Na Amran Kaima

Toa comment