The House of Favourite Newspapers

Mastaa Wasusia Maziko Ya Bi Cheka Bunju B, Dar (Picha +Video)

0

VILIO, majonzi na simanzi, jana Ijumaa Novemba 29, 2019 vilitawala katika kila kona maeneo ya Bunju B jijini Dar, wakati wa maziko ya aliyekuwa msanii maarufu wa Bongo Fleva, Cheka Hija ‘Bi Cheka’ (60) , Risasi Jumamosi lilishiriki shughuli hiyo.

 

Kubwa lililojitokeza ni wasanii kususia tukio hilo la kumpumzisha kwenye nyumba yake ya milele mwenzao huyo ambaye walifanya naye kazi bega kwa bega.

 

Mazishi hayo yalihudhuriwa na umati mkubwa wakiwemo ndugu ambao ni wajukuu aliokuwa akiwalea.

Miongoni mwa waliofurika kwenye msiba huo ni vijana waliotarajia kuona sura mbalimbali za mastaa ambao hawaonekani kirahisi mpaka kwenye matukio makubwa.

 

Kundi la waliotarajia kuwaona mastaa kwenye msiba huo liliishia kuwaona Dogo Aslay, Beka Flavour na Temba tu.

Hata hivyo, hata hao walionekana wakiwa kwenye ulinzi mkali wa mabaunsa wao.

Mabaunsa hao walitaka kuvuruga hali ya hewa msibani hapo baada ya kijana mmoja kuwapiga picha wasanii hao ambapo lilitokea varangati la muda kabla ya kutulizwa na watu wazima wakiomba kumpisha shetani apite.

 

Wanahabari wetu waliwafuata wasanii hao ili kusikia walivyoguswa na msiba huo, lakini alitokea jamaa waliyekuwa naye kama baunsa na kukataza wasanii hao kuhojiwa akisema waachwe kwani hawana nguvu ya kuzungumza kutokana na pigo la kuondokewa na Bi Cheka.

Akizungumza na mwandishi wetu, mtoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Kombo Shabani alisema kuwa, mama yake alizaa watoto tisa ambapo wengine walifariki dunia na kubaki mmoja.

 

Safari ya maisha ya Bi Cheka iliishia kwenye Makaburi ya Kihonzile, Bunju B jijini Dar ambapo mwili wake ulipumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.

Bi Cheka amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 61 ambapo alipata umaarufu mwaka 2012 alipoingia kwenye muziki wa Bongo Fleva akiwa kama msanii chipukizi.

Kufuatia umri wake kuwa mkubwa, ndani ya muda mfupi alipata umaarufu baada ya kuachia wimbo wake wa Ni Wewe alioshirikiana na Mheshimiwa Temba.

STORI: RICHARD BUKOS NA MEMORISE RICHARD

MAZISHI YA BI CHEKA: BARABARA ZAFUNGWA, UMATI WAFURIKA KUMZIKA!

Leave A Reply