The House of Favourite Newspapers

Mastaa Watakavyosherekea Krismasi

0

 

MSIMU wa sikukuu za kufunga mwaka ndio huu, leo tunasherehekea siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo maarufu kama Krismasi na Jumanne ijayo, itakuwa ni sikukuu ya Mwaka Mpya 2020.

Kwa mwaka mzima, watu wanakuwa wameweka mikakati yao ya kimaendeleo na inapofika mwishoni kama hivi, wanajipongeza kwa kile walichokivuna.

 

Ndio maana Wachaga wamekuwa na desturi ya kwenda kwao, kukaa pamoja na ndugu zao lakini wengine husherehekea kwa namna tofautitofauti.

Makala haya yanakuletea orodha ya baadhi ya mastaa wakifunguka namna ambavyo watakula sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya:

 

SLIM OMARY-MUIGIZAJI

“Krismasi hii nitakuwa Hororo mpakani mwa Kenya na Tanzania na nitakuwa huko nikilima kwa kuwa Mungu alisema asiyefanya kazi na asile, hivyo ninasherehekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo nikiwa nafanya kazi.”

 

BARNABA-BONGO FLEVA

“Krismasi hii nitakuwa kwenye shoo zangu za Moshi, Tanga, Mtwara, Dodoma na Arusha. Hivyo kwa upande wangu itakuwa ni sikukuu ya majukwaani. Siku ya mkesha wa Krismasi nitakuwa Mtwara, Krismasi yenyewe nitakuwa Dodoma, baada ya hapo nitakwenda Tanga na baada ya Tanga nitakuwepo Arusha.”

 

PETER MSECHU-BONGO FLEVA

“Sikukuu hii ya Krismasi nitakuwepo nyumbani nikisherehekea kuzaliwa kwa Yesu nikiwa na familia yangu.”

 

YUSUPH MLELA-MUIGIZAJI

“Unajua sikukuu siku zote ni siku ya upendo na kuwa karibu zaidi na familia, kwa hiyo nitakuwa na familia yangu nyumbani Kinondoni halafu baadaye mida ya jioni nitatoka na mpenzi wangu. Bado sijajua itakuwa kiwanja gani, tutajua siku hiyohiyo.”

 

BILNASS-BONGO FLEVA

“Sikukuu hii nitakuwa mikoani kama Babati, Mto wa Mbu, Karatu na Singida yaani kuanzia tarehe 24 mpaka Januari 2 mwakani nitakuwa nikitembelea hiyo mikoa na nitakuwa nikitoa burudani kwa mashabiki zangu, hivyo ndivyo nitakavyosherehekea Krismasi na Mwaka Mpya.”

 

AMBER LULU-BONGO FLEVA

“Sikukuu hii imenikuta safarini lakini nafurahi maana itakuwa ni bata mwanzo mwisho. Nitakuwa Mbeya nikifanya shoo pamoja na wasanii wenzangu; Diamond Platnumz na Rayvanny kwenye Uwanja wa Sokoine. Mwaka Mpya bado sijajua lakini naamini itakuwa poa tu.”

 

VINCENT KIGOSI-MUIGIZAJI

“Krismasi hii bwana kwangu mimi itakuwa ya tofauti kidogo. Nitatoka Bongo, nitakuwa na familia yangu yaani mke wangu pamoja na mtoto wetu kwenda huko shamba Zanzibar.”

 

MBOSSO-BONGO FLEVA

“Krismasi hii nimepanga kuwapa burudani mashabiki zangu kwenye jukwaa la Dar Live na ninaamini hawatojutia kulipia kiingilio chao kwani nimewaandalia mambo mazuri sana. Ninachowaomba wajiandae vizuri kupokea burudani ya kukata na shoka kutoka kwangu.”

 

AMINI-BONGO FLEVA

“Krismasi hii nitakuwepo tu mjini hapa pamoja na familia yangu tukisherehekea kwa pamoja, tutakula tutakunywa na tutafurahi kwa pamoja.”

 

MAKALA: Irene Marango

Leave A Reply