The House of Favourite Newspapers

MASWALI TATA UPATIKANAJI WA MO

Related image
Mohammed Dewji ‘Mo’

SHANGWE za kupatikana kwa mfanyabishara bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ Jumamosi iliyopita baada ya kutekwa na wasiojulikana ziko kila mahali nchini, lakini nyuma ya tukio hilo watu wengi wamejaa maswali tata, Ijumaa Wikienda limebaini.  

Kwa mujibu wa mitandao mbalimbali ya kijamii, mazungumzo mitaani na uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa licha ya Mo kupatikana, bado vyombo vya usalama vina kazi ya kufanya ili kuweza kujibu maswali ambayo mengi kati yake yanakosa majibu na hivyo kuwaweka watu njia panda juu ya kile kilichomkuta mfanyabiashara huyo kijana.

Siku chache zilizopita baada ya watekaji kuondoka na Mo kusikojulikana, wengi walijiuliza: “Kina nani wamemteka. Sababu ni nini, kwa nini hawajakamatwa na je, Mo angepatikana akiwa mzima au amekufa?” Juzi (Jumamosi) alfajiri baada ya Mo kupatikana majibu mengi ya maswali yalipatikana na hivyo kuwafanya wengi kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii kutoa shukrani zao kwa Mungu kwa kuwezesha mfanyabiashara huyo kupatikana akiwa hai.

Awali ilionekana kuwa, pengine upatikanaji wa Mo ungehitimisha mijadala ya tukio hilo na kuwafanya watu kuendelea na maisha mengine, lakini ghafla yakazuka tena maswali juu ya mazingira ya upatikanaji wake. Ukiweka kando maswali ya wakosoaji wa kila kitu ambao kwao kutafuta makosa ndiyo kazi yao, watu wengine walijiuliza: “Ilikuwaje watekaji watelekeze gari pamoja na silaha zao tena katikati ya jiji na kumwacha mateka wao aende kirahisi?

Hoja juu ya swali hilo ni kwamba imezoeleka watekaji kuwatupa mateka wao nje ya mji ili wachelewe kupata msaada na wao kupata nafasi ya kutokomea, lakini kwa Mo haikuwa hivyo, jambo lililowafanya wengi kudhani kuwa huwenda watekaji wako mjini ndiyo maana hawakuhitaji muda mwingi wa kutokomea na silaha za kubeba kujilinda. Swali jingine tata ni je, watekaji hao waliondokaje eneo la tukio baada ya kutelekeza gari au walikuwa na usafiri mwingine?

Na kama walikuwa nao ni wa nani? Maana taarifa zinadai kuwa waliomteka Mo wanasadikiwa kuwa ni raia wa kigeni na kwamba waliingia nchini mwezi mmoja uliopita na gari lao kwa shughuli isiyoelezwa wazi. Aidha, taarifa za kipolisi zilidai kuwa watuhumiwa walijaribu kulichoma moto gari hilo, lakini haikuwezekana, jambo ambalo nalo lilizua utata juu ya kushindwa kwao kwani gari linalotumia mafuta aina ya petroli ni rahisi kulichoma na hivyo kuifanya nia ya kuliteketeza gari waliyotaka kuifanya kukosa mashiko.

Kama hayo hayatoshi, taarifa za vyombo vya usalama zinadai kuwa, sababu ya Mo kutekwa ni watuhumiwa kutaka kujipatia fedha, lakini hata hivyo, fedha hawakupata jambo ambalo linazua swali tata; ilikuwaje wamwachie bila nia yao kutimia? Maswali haya na mengineyo yanavipa kazi vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuendelea kufanya kazi ya ziada ili kuja na majibu ya utata wa tukio la Mo kutekwa na kupatikana katika mazingira tatanishi na kazi hiyo ni kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kuwa, tangu kutekwa kwa Mo hadi kupatikana kwake wasemaji wa Serikali kuhusu tukio hilo wamekuwa wengi jambo ambalo wakati mwingine liliongeza mkanganyiko hasa baada ya taarifa ya chombo kimoja cha usalama kushindwa kupita njia moja ya maelezo na chombo kingine na hivyo kuwafanya watu waulizane nani wa kumwamini!

Kufuatia kuwepo kwa mpishano mdogo wa taarifa za Mo kutekwa kutoka kwenye vyombo husika wengi wameshauri kuwa, ni vyema linapotokea tukio kubwa kama hilo msemaji akawa ni mmoja ambaye ataulisha umma habari zisizokuwa na mkanganyiko hivyo kutozua maswali kama yalivyo sasa.

STORI: Mwandishi Wetu, DAR

Masaa 3 Lema Kuhojiwa POLISI Kuhusu MO Atoka na Kutema cheche

Comments are closed.