The House of Favourite Newspapers

Mauaji Yamchefua Rais Samia, Dkt. Mpango Amtumia Salam IGP Sirro

0

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema amesikitishwa na kuumizwa kutokana na matukio ya mauaji yanayotokea nchini, na kuliagiza Jeshi la Polisi kupitia Idara ya Intelijensia kukomesha matukio hayo.

 

Aidha, ametoa siku saba kwa jeshi hilo kuwasaka waliohusika na mauaji ya watu watano wa familia moja na taarifa ya kazi hiyo zifikishwe kwake. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema hayo alipozungumza kwa niaba ya Rais Samia, alipofika Kijiji cha Zanka wilayani Bahi mkoani Dodoma kwa ajili ya kutoa pole kwa familia iliyofiwa na watu watano.

 

“Kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan nimekuja kutoa pole kwa familia ambayo imekatiliwa sana kwa kuuawa watoto wao, kutoa pole pia kwa Kijiji cha Zanka. Mheshimiwa Rais amesononeka sana, tukio hili la kikatili na la kinyama linaumiza sana,” alisema Makamu wa Rais.

 

Dk Mpango alisema Rais Samia na serikali kwa ujumla wamechoshwa na matukio ya mauaji ambayo yamekuwa yakitokea na kulitaka Jeshi la Polisi kukomesha matukio hayo kwa kuyazuia mapema.

 

“Nifikishe salamu kwa IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini) haya mauaji nchi nzima yakome, mkafanye kazi yenu sawa sawa, mkafanye kazi ya kuyazuia,” alisema Dk Mpango akimwambia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga kufikisha salamu hizo za IGP Simon Sirro.

 

“Haiwezekani Zanka watano wa familia moja, Moshi mama kauawa na kutupwa chooni mtuhumiwa ni binti yake, Mbeya hayo hayo baba ameuawa mtuhumiwa ni mwanaye mwanajeshi, leo (jana) mchana huu nimesikia kijana ameuawa, baadhi ya polisi ni watuhumiwa, Mwanza kuna watu wameuawa, hatuwezi kwenda hivi kama nchi hata kidogo,” alisema Makamu wa Rais akirejea baadhi ya matukio ya mauaji yaliyoripotiwa hivi karibuni nchini.

 

“Jeshi la Polisi mna kazi kubwa ya kufanya nchi nzima, Kiongozi na Amiri Jeshi Mkuu amechoka, mimi nimechoka, hatuwezi kuongoza nchi ambayo ni mauaji kila mahali.” Makamu wa Rais hakuishia hapo, aliongeza: “Jeshi la Polisi na idara zake wafanye kazi usiku na mchana kuzuia uhalifu wa namna hii ambao ni mbaya sana, na hao wanaohusika katika hiyo mikoa mingine Jeshi la Polisi lisijisafishe.

 

Najua Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri, lakini wapo watu wachache wamo humo ndani wanaharibu sura ya jeshi. Intelijensia ndani ya Jeshi la Polisi ifanye kazi yake.” Kuhusu mauaji ya watu watano wa familia moja, Dk Mpango ambaye pia alikabidhi rambirambi kwa wafiwa, alisema tukio hilo linatisha na kuumiza na kutoka siku saba kuanzia jana, taarifa za tukio hilo zinafika ofisini kwa Rais Samia.

 

“Hili tukio linatisha na linaumiza sana, niko hapa kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan amenituma niwape pole, Mwenyezi Mungu awafariji. Tukio kama hili halikubaliki kabisa katika nchi hii,” alisema Dk Mpango.

 

“Pamoja na hatua ambazo zimechukuliwa na mkuu wa mkoa, ninatoa maelekezo vyombo vyote vifanyie kazi mauaji haya mara moja na taarifa ndani ya siku saba kuanzia leo (jana) taarifa rasmi iwasilishwe kwa mheshimiwa Rais, hali hii haikubaliki hata kidogo,” aliongeza Dk Mpango.

 

Dk Mpango amehimiza vyombo vya ulinzi kufanya kazi yao kwa weledi na kuwasaka wahusika wote wa matukio na kufikisha kwenye vyombo vya sheria.

 

“Hatuwezi kwenda namna hii na niseme mapema Idara yetu ya Upelelezi ihakikishe inakuwa hapa saa 24 na vyombo vingine vyote msaidiane kuhakikisha hawa watu wanapatikana.

 

“Muwasake wahusika wote ili wakawe mfano kwa watu wengine, mtoto wa form one (Kidato cha Kwanza) kakosa nini, mtoto wa darasa la nne kakosa nini, ni unyama wa ajabu. Kamanda wa Polisi watu wako mhamie hapa mfanye hiyo kazi na mlete taarifa ndani ya siku saba,” alibainisha.

 

Dk Mpango pia alitoa rai kwa viongozi wa dini kusaidia kuwakumbusha waumini wao wajibu wao kwa Mungu na kwa mwanadamu na kusisitiza kuwa hakuna binadamu mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa binadamu mwingine.

 

“Kama una matatizo na jirani au ndugu yako zipo njia, wapo wazee, serikali ipo, viongozi wa dini mkatukumbushe wajibu wetu kwa Mungu na binadamu wenzetu, hata simba hawauani sasa wanadamu tumegeuka waovu,” alisema Dk Mpango.

 

Pia, amewataka viongozi wa chama na serikali katika ngazi zote kufanya mikutano ya mara kwa mara na wananchi na kuweka nguvu katika kuhimiza usalama wa wananchi na mali zao.

Leave A Reply