The House of Favourite Newspapers

Mauzauza Eneo la Ajali Iliyoua watu 26 Mkuranga

PWANI: Kufuatia watu 26 kufariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa baada ya basi dogo (Hiace) lililokuwa likitoka Mkuranga kuelekea Kimanzichana mkoani Pwani, kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba chumvi likitokea Mtwara kuelekea Dar es Salaam, dereva mmoja ametoboa siri ya kuwepo kwa mauzauza.

 

Akizungumza na gazeti hili eneo la tukio dereva wa lori linalofanya safari zake kati ya Dar na mikoa ya Kusini, aliyejitambulisha kwa jina la John Bisho alisema eneo hilo karibu na Kijiji cha Mparange lina mauzauza.

 

“Ni eneo ambalo maredeva hawatakiwi kwenda kwa mwendo kasi kwa sababu mimi mara mbili hivi niliwahi kuona giza wakati naendesha, bahati nzuri ni kwamba mwendo wangu ni mdogo na hakukuwa na gari nililopishana nalo,” alisema Bisho huku akiungwa mkono na utingo wake ambaye hakutaka kujitambulisha jina.

Eneo la tukio.

 

Ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia Jumapili Machi 25, 2018 katika kijiji hicho cha Mparange,Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.Naye shuhuda mmoja, Said Kiloga alisema yeye anaamini kwamba ajali hiyo ilitokana na mwendo kasi kwa magari yote yaliyohusika na ajali hiyo.

 

“Magari yote yalikuwa kwenye mwendo wa kasi kupita kiasi, kwa kweli nilipopitwa na basi ndogo leye usajili namba T 676 DGK, kufumba na kufumbua nikashuhudia magari yakigongana uso kwa uso na kishindo kikubwa kilitokea,” alisema Said ambaye alisema yeye ni mgeni tu kijijini hapo.

 

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Kibiti, ACP Mohamed Likwata, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, alipoulizwa majeruhi wako wangapi mkuu huyo wa polisi alikuwa na haya ya kusema:

Miili ya marehemu ikizikwa.

“Ni kwamba majeruhi wote zaidi ya 10 wamepelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam ambako wanaendelea kupata matibabu.”Juzi, Rais Dk John Magufuli alimtumia Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, rambirambi kutokana na vifo vya watu hao 26.

STORI: MWANDISHI WETU, UWAZI

Comments are closed.