The House of Favourite Newspapers

Mawakala wa bandari sasa kulipa kwa elektroniki

0

1.
Kaimu Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Kilian Chale (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano na wanahabari leo Ijumaa, Oktoba 9, 2015. Kushoto kwake ni Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano, Focus Mauki.
2.Viongozi hao wakisikiliza maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wanahabri(hawapo pichani).Viongozi wa TPA wakisikiliza maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wanahabari (hawapo pichani) wakati wa mkutano wao uliofanyika leo Ijumaa, Oktoba 9, 2015.
3.Wanahabari wakifuatilia mkutano huo.Wanahabari wakifuatilia mkutano huo baina yao na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) uliofanyika leo Ijumaa, Oktoba 9, 2015.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeachana na mfumo wa zamani wa karatasi na badala yake wateja ambao ni mawakala wa kutoa mizigo bandarini sasa wataanza kutumia huduma za malipo kupitia simu za mkononi, Visa Card na Master Card kulipia gharama.
Kaimu Mkurugenzi Teknolojia ya Mawasiliano na Habari, Kilian Chale, amesema hayo wakati wa mkutano wake na wanahabari uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dar es Salaam leo.
Amesema mfumo huo wa malipo kwa njia ya elektroniki (IePS) uliozinduliwa Julai mwaka huu ni mzuri, salama na unarahisisha kazi kwa kupunguza misongamano kwa wateja, hivyo kusaidia kukuza uchumi.
Chale ametoa wito kwa mawakala wa mizigo kuendelea na usajili wa kutumia mfuo huo ili kurahisisha na kuharakisha kazi ya kutoa mizigo bandarini, hatua ambayo itaongeza ufanisi wa mamlaka hiyo katika kuhudumia wateja wake.
“Mawakala wengi wameanza kutumia mfumo huu ambao tayari umeunganishwa na Benki za CRDB, NMB na Benki ya Posta ili kumwezesha wakala kupata ankara ya malipo, kufanya malipo na kisha kwenda moja kwa moja katika eneo la kuchukulia mizigo ndani ya bandari,” amesema Chale.
Amesema, wakala anaweza kutumia Benki ya CRDB kufanya malipo kwa kutumia CRDB SimBanking, CRDB Internet Banking, CRDB fahariHuduma, NMB Internet Banking, NMB Mobile Banking na pia anaweza kutumia matawi ya CRDB, NMB na Benki ya Posta.
Hata hivyo, alifafanua kuwa ili kuutumia mfumo huo wakala anapaswa kusajiliwa na mamlaka kwa kwenda ofisini au anaweza kujisajili mwenyewe kupitia tovuti rasmi ambayo ni www.tpapayments.com.
“Mteja wa kawaida pia anaweza kuingia katika tovuti hii na kuona ankara ya malipo ya huduma za bandari kwa kila mzigo au gari aliloagiza,” alisema Chale na kuongeza kwamba, mfumo huo utaweka uwazi na kupunguza kwa kiwango kikubwa malalamiko ya wateja ya kukosa taarifa sahihi za gharama za mizigo yao.

NA DENIS MTIMA/GPL

Leave A Reply