The House of Favourite Newspapers

Mayanga: Siwachukii Wachezaji wa Yanga

0
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga.

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga, ameeleza kusikitishwa na uongo unaoendelea kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa anawachukia wachezaji kutoka Yanga akidai anaamini Mungu atamlipia kwa yeyote anayehusika kumchafua.

Akizungumza na ABM FM Radio ya Dodoma kwa njia ya simu akiwa mjini Mwanza, Mayanga amesema uzushi wote unaoenezwa juu yake kupitia mitandaoni anaufahamu ila hajui wanaomzushia wana ajenda gani dhidi yake.

Kwenye ujumbe huo kuna madai kuwa kocha huyo wa Stars amekuwa akiwatisha wachezaji wanaowindwa na Yanga kuwa kama watakubali kusajiliwa na timu hiyo, hatawateua tena kuchezea Stars.

“Wakati nilipokuwa msaidizi wa Mart Nooij mimi ndiye niliyemshauri tukateua wachezaji tisa kutoka Yanga. Wanayanga waukubali ukweli juu ya kikosi chao, angalia beki wa kati, alikuwa Bossou, kwenye viungo kuna Kamusoko na Niyonzima, wakati safu ya ushambuliaji ni Ngoma, Tambwe na Chirwa, pale nifanyeje kama si kunionea?” alihoji Mayanga.

Kocha huyo wa Stars amesema kwa kutambua upungufu kwenye safu ya ulinzi, alimuomba Kelvin Yondani aje kuimarisha nguvu lakini beki huyo aliombwa aachwe ili akamilishe kwanza mipango ya ndoa yake.

Mayanga aliongeza kuwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Haji Mwinyi, Salum Makapu na Aggrey Morris inakuwa vigumu kuwaita baada ya Zanzibar kupata uanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Stars juzi iliwatibua Watanzania baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Rwanda katika michuano ya kufuzu Chan kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Leave A Reply