The House of Favourite Newspapers

Mazembe yampa Samatta ulaji mwingine

1

Samata-vs-MalawiMchezaji wa TP Mazembe, Mbwana Samatta.

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
MAMBO yanazidi kunoga kwani TP Mazembe sasa inataka kumuuza straika wake Mbwana Samatta kwa timu ya Standard Liege baada ya RC Genk kuonekana wana fedha kiduchu.

Hadi wiki iliyopita wakati wa sikukuu ya Krismasi, Mazembe ilikuwa ikizungumza na Genk pia ya Uturuki lakini klabu hiyo ilishindwa kulipa dau la euro milioni 2.5 (Sh bilioni 5.7), ikawa inataka ipunguziwe.

SamataBwana580211.jpgBosi wa Mazembe, Moise Katumbi alisafiri hadi Ubelgiji ili kufanikisha usajili huo, lakini Genk wakaonekana kama wanasuasua hali iliyomlazimu kurudi DR Congo na kumuacha wakili wake.

Mazembe ilikataa ofa ya Genk ambayo ni pungufu kwa ile aliyotaka Katumbi na hata walipotoa ya pili bado mambo yakawa vilevile.

Baada ya kuona longolongo zinakuwa nyingi kwa Genk, Mazembe sasa inataka kumuuza Samatta kwa Standard Liege na jana Ijumaa kutwa nzima maofisa wa Mazembe walikuwa jijini Dar es Salaam wakizungumza na Samatta kuhusu ofa hiyo mpya.

Ofisa mmoja wa mmoja wa Mazembe, amelithibitishia Championi Jumamosi kuwa, Mkurugenzi wa Michezo wa Mazembe, Frederick Kitenge na wakili wa timu hiyo wapo jijini Dar es Salaam kuweka mambo sawa.

“Dau la Genk limeonekana kuwa dogo na Katumbi hataki kukubali ofa yao, hivyo sasa mambo yamebadilika na mazungumzo yaliyopo ni Samatta kujiunga na Standard Liege.

“Hadi sasa (jana Ijumaa saa 9:30 alasiri) bado wanazungumza na Samatta na wawakilisha wengine ili kukamilisha mipango ya kumuuza kwa Standard Liege, inaonekana itakuwa na fedha nzuri zaidi ya Genk.
“Kazi kubwa wanayoifanya ni kukubaliana kwanza kuhusu ofa hiyo mpya, kama mambo yakienda vizuri yatavunjwa makubaliano ya awali ya Samatta na Genk halafu ndiyo asaini mkataba mwingine mpya.

“Standard Liege wapo tayari kutoa zaidi ya euro milioni 2.5 (Sh bilioni 5.7) ndiyo maana Katumbi anataka kumuuza kwao na siyo Genk, hapa ni mambo ya fedha tu na kucheza na hesabu,” alisema ofisa huyo.
“Samatta ni kama ameduwaa, ila uamuzi ni wake mwenyewe kama anataka Genk au Standard Liege ila ili kuweka uhusiano mzuri na Mazembe, inaonekana atamsikiliza Katumbi anachotaka.”

Alipotafutwa wakala wa Samatta, Jamal Kisongo alisema; “Ni kweli kuna kitu kama hicho ila bado tupo katika mchakato hapa.”

Standard Liege maarufu kama The Reds iliyoanzishwa miaka 117 iliyopita, si timu ya kubeza kwani inacheza Ligi Kuu ya Ugiriki na ipo nafasi ya nane huku Genk ikiwa nafasi ya saba.
Timu hiyo inayonolewa na Yannick Ferrera inatumia Uwanja wa Maurice Dufrasne unaoingiza mashabiki 28,272, Januari 20, mwaka huu itacheza na Genk katika muendelezo wa Ligi ya Ugiriki.
Standard Liege imeshiriki mara 11 Ligi ya Mabingwa Ulaya na kucheza mechi 43 kati yake ikishinda mechi 23, sare sita na kufungwa mara 17, katika Kombe la Ulaya imeshiriki mara sita na kucheza mechi 36, imeshinda mara 19, sare tano na kufungwa mara 12.
Moja kati ya mafanikio ya Standard Liege ni kufika fainali ya Kombe la Europe katika msimu wa 1981/82 lakini ikafungwa mabao 2-1 na Barcelona.

1 Comment
  1. Mussa says

    Standard ni timu kubwa na ina washabiki wengi ni kama Yanga. Samatta anaweza kusaini bila shaka lakini awe makini saana kwa vipengele khaza kama muda wa contrat asizidishe miaka mitatu, akitaka kununuliwa na timu nyingine asizidishe ×2 bei wametoa kwa mazembe. Juu ukijibana kwenye mukataba wako timu inaweza kukuzorotesha mpaka unakwisha kabisaa
    Kwa hio kama mutampa ujumbe Samatta ao analipa Mbokani wa Norwich aliceza sana uko na samatta watampenda sana

Leave A Reply