The House of Favourite Newspapers

Mazishi Familia Moja Waliokufa Kwa Moto Yaacha Simanzi

0

SIMANZI na vilio vilitanda Jumanne katika mazishi ya familia moja ya Sigfrid Kimbi (44) iliyoteketea kwa ajali ya moto huko Sahare mkoani Tanga na kusababisha vifo vya watu wanne.

 

Mazishi hayo yaliyofanyika katika kitongoji cha Kisomboko-kata ya Uru Kusini wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, yaliacha vilio kwa waombolezaji hasa ikizingatiwa familia nzima imeteketea.

Wakizungumza na RISASI kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi waliohudhuria mazishi hayo, walisema tukio hilo limewashtua kwa sababu haijawahi kutokea familia nzima kupoteza maisha.

 

“Hii ilikuwa ni familia yenye upendo wa dhati hata kwa majirani zake, kwa sababu kama tulivyoelezwa kuwa huyu baba alirudi ndani kujaribu kuwaokoa wanawaye na mkewe, lakini bahati mbaya alipata majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake,” alisema Augusti Kimaro.

 

Pia Martha Chuwa naye alisema tukio hilo limeleta simanzi nzito hapo kijijini na kuongeza kuwa taasisi za serikali zinatakiwa kuchukua hatua haraka pindi zinapopewa taarifa za hitilafu ya umeme.

“Kwa sababu tunasikia hiyo nyumba ilikuwa na hitilafu ya umeme, waliripoti Tanesco lakini hawakuchukua hatua hadi shoti kubwa ilipotokea na sasa imechukua hawa ndugu, kwa kweli inauma sana,” alisema.

KAMANDA HUYU HAPA

Aidha, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda alisema tukio hilo lilitokea Disemba 26, mwaka huu muda wa saa 11 alfajiri.

Alisema ajali hiyo ya moto ilitokea katika nyumba waliyokuwa wakiishi marehemu katika mtaa wa Sahare Majengo Mapya kata ya Mzingani jijini Tanga.

Aidha, aliwataja marehemu kuwa, Sigfrid Kimbi (44) ambaye alikuwa baba wa familia, mkewe Aurelia Shayo na wanawe Samweli Kimbi (9) na Ezra Kimbi (7).

Alisema mke na watoto hao walifariki papohapo wakati baba wa familia hiyo, alifariki katika Hospitali ya Bombo wakati akipatiwa matibabu.

 

Alisema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme na kuongeza kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.

Leave A Reply