The House of Favourite Newspapers

Mazishi Kigogo wa Viroba Aliyejipiga Risasi Yafichua Mambo

Na MWANDISHI WETU| GAZETI LA UWAZI| HABARI

DODOMA: Tukio la mfanyabiashara mkongwe mkoani hapa, Festo John Mselia (64) kujiua kwa kujipiga risasi ya kichwani na kuharibu ubongo bado liko midomoni mwa watu, kikubwa ni mambo yaliyofichuka kufuatia kifo hicho, Uwazi linakupa zaidi.

SIKU YA TUKIO KWANZA

Festo aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa wa vinywaji, alijiua kwa risasi ya bastola, Machi 7, mwaka huu kwenye shamba lake lililopo eneo la Miuji mkoani hapa.

SABABU ZINAZOJULIKANA

Sababu iliyotawala vichwani mwa watu ya marehemu Mselia kujitoa roho ni kitendo cha Polisi Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Kamanda wa Polisi, ACP Lazaro Mambosasa, kukamata shehena kubwa ya pombe za viroba vya thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja kwenye ghala lake mjini Dodoma.

YALIYOJIRI KABLA YA KUJIUA

Machi 10, wakati wa kuuaga mwili wa marehemu huyo kwenda mkoani Kilimanjaro kwa mazishi, Uwazi lilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya marafiki wa karibu na marehemu ambao walisema kuwa, baada tu ya kusikia, ghala la Mselia limevamiwa na polisi na shehena ya viroba vimekamatwa, walimpigia simu ili kutaka kukutana naye na kumtia nguvu lakini hakupokea.

“Mimi marehemu alikuwa rafiki yangu sana. Nilipewa taarifa na vijana wangu wa kazi kwamba, polisi wamevamia kwenye ghala lake la viroba na kukamata shehena yote.

“Kijana wangu aliniambia kwamba, polisi walimpa maelekezo Mselia asiuze hata boksi moja lenye viroba mpaka wa TFDA (Mamlaka ya Dawa na Chakula Tanzania) wafike na kumpa maelekezo.”

ALIKUWA MTU WA MAAMUZI YA HAPOHAPO

“Kama nilivyosema alikuwa rafiki yangu, kusikia hivyo niliamua kumpigia simu yake ya mkononi, lengo langu ni kutaka kukutana naye, kumpa pole na pia kumtia nguvu asilichukulie jambo lile kama ni mwisho wa kutafuta. Lakini akawa hapokei simu.

“Marehemu alikuwa mtu wa maamuzi ya hapohapo, siku zote alikuwa akitaka kufanya jambo hapendi kupindishwa mawazo na mtu. Akisema anataka kufanya jambo, lazima alifanye. Alikuwa akisema anataka kukopa benki ni mpaka apate mkopo ndipo anaweza kusikiliza mawazo mengine,” alisema rafiki huyo.

Wazee wengine watatu wa Dodoma, akiwemo mmoja mmiliki wa baa maarufu aliyeomba asitaje jina lake wala la baa, walisema wao pia walimpigia simu muda mfupi baada ya polisi kumaliza kuongea naye.

“Mimi nilikwenda mpaka kwenye ghala, maana alinitumia ujumbe wa simu, kufika nikakuta kuna askari, nikaondoka kwa nia ya kumtafuta baadaye. Baadaye nilipompigia simu akawa hapokei,” alisema mmiliki huyo wa baa.

MAREHEMU NA POLISI SAA 10 JIONI

Habari zaidi zinasema kuwa, mpaka Kamanda Mambosasa anamaliza kuongea na mzee Mselia ilikuwa saa kumi jioni, akaingia ndani ya gari lake lakini hakuendesha yeye, alimwomba rafiki yake (jina halikujulikana) amuendeshe kwenda kwenye mashamba yake.

“Ilikuwa ni kawaida kwa mzee Mselia kwenda kwenye mashamba yake yaliyopo Miuji, njia ya kwenda Kondoa. Kule kuna shamba lenye mifugo na mazao. Kufika, yeye alishuka, aliyekuwa akimwendesha alibaki kwenye gari.

“Lakini akasema kuwa, pia atakwenda shamba la mazao ambalo umbali wake ni kwa mwendo wa baiskeli,” alisema ndugu mmoja wa marehemu.

SAA 1 JIONI, ALIYEGUNDUA AMEJIPIGA RISASI

Kwa mujibu wa ndugu huyo, mfanyakazi wa shambani ndiye aliyemkuta mzee Mselia akiwa anagaagaa kwenye shamba hilo tayari amejipiga risasi kichwani.

“Unajua iko hivi, yule dereva aliona muda unakwenda mzee Mselia harudi. Ilikuwa saa moja jioni, akamtuma mfanyakazi wa marehemu (shamba boi) amfuate.

“Shamba boi alichukua baiskeli na kumfuata kule. Kufika, akamkuta Mselia yupo chini anagalagala, damu zinamtoka kichwani. Mfanyakazi alikimbia kwenda kumweleza aliyekwenda naye. Kwa hiyo, mfanyakazi ndiye aliyemwona marehemu kwa mara ya kwanza akiwa ameshajipiga risasi,” alisema ndugu huyo.

HAKUNA ALIYESIKIA MLIO WA BASTOLA?

Ndugu huyo alisema kuwa, hakuna aliyesikia mlio wa risasi kutokana na umbali kati ya shamba la mifugo walikofikia na gari na shamba la mazao alikokwenda marehemu na kujiua.

MWILI WAAGWA, WATU WAHOJI

Mwili wa marehemu Mselia uliagwa katika Kanisa la Romani Katoliki Uwanja wa Ndege ambapo inasemekana kuwa, baadhi ya watu walihoji kulikoni mtu aliyejiua kuagwa kanisani?

PADRI AKEMEA

Hata hivyo, padri aliyeendesha ibada hiyo ambaye anatajwa kwa jina la Erick alikemea tabia ya watu kujichukulia maamuzi ya kujitoa uhai.

Padri huyo kwenye ibada hiyo alisema, mbali na yeye kutopenda maamuzi hayo, kanisa pia msimamo wake halikubaliani na tabia za wanadamu kujiua wenyewe.

WAZEE WA KIMILA

Mwili wa marehemu Mselia ulizikwa Jumamosi iliyopita kijijini kwake, Kichori, Kibosho Umbwe Moshi, mkoani Kilimanjaro ambapo baadhi ya wazee wa kimila walisema kuwa, zamani za wazee wao, mtu akijiua hufanywa tambiko maalum kwa ajili ya kuondoa kumbukumbu mbaya katika familia.

“Lakini kwa sababu miaka hii mambo ya tambiko hayapo, ni muhimu familia ikaandaa ibada maalum ya kuiombea familia ya marehemu ili kuondokana na taswira ya tukio hilo,” alisema mzee aliyejitambulisha kwa jina moja la Masawe.

Marehemu Mselia ameacha mke na watoto watano, wakiwemo watatu wa kike.

SHINDA NYUMBA YA AWAMU YA PILI YATIKISA JIJI LA DAR ES SALAAM

Comments are closed.