KLABU ya Mbao ya jijini Mwanza imekabidhiwa basi lenye thamani ya Sh70 milioni kwa ajili ya wachezaji. Basi hilo wamekabidhiwa leo Jumatano na wadhamini wao Kampuni ya GF Truck and Equipments katika makao makuu ya kampuni hiyo yaliyopo Vingunguti, Dar es Salaam.
Mbao inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi sita, huku Simba ikiwa kileleni na pointi 12 ikifuatiwa na Yanga ambayo ndiyo mabingwa watetezi wakiwa na tofauti katika mabao ya kufunga na kufungwa.
Mkurugenzi wa GF, Alijawad Karmali, alisema basi hilo ni sehemu ya mkataba ambao waliingia na Mbao miezi miwili iliyopita. Mbunge wa Nyamagana, Angelina Mabula, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo na aliishukuru Kampuni ya GF Trucks kwa kutimiza ahadi yao kwa Mbao.
Mabula ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi, Maendeleo ya Nyumba na Makazi, alisema baada ya kuingia mkataba na kampuni hiyo wameanzisha kampeni ya ubingwa ili kulitoa taji kwa timu za Mkoa wa Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njashi, alisema wanawashukuru GF kwa udhamini huo mkubwa waliouweka kwani mpaka basi hilo wanalipokea katika mikono yao limezidi thamani ya Sh70 milioni, kwani wamelipokea likiwa limelipiwa kila kitu.
(PICHA: MUSA MATEJA | GLOBAL PUBLISHERS)