The House of Favourite Newspapers

Mbaroni kwa Tuhuma za Kusafirisha Wahamiaji Haramu

0

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani, limemkamata dereva wa gari lenye namba za usajili T 703 DTR aina ya Hiace, mkazi wa Uyole Mbeya akituhumiwa kisafirisha wahamiaji haramu sita raia wa Malawi.

 

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa, alisema dereva huyo ambaye jina linahifadhiwa alikamatwa juzi katika eneo la Tanita Wilaya ya Kibaha majira ya saa nne asubuhi akitokea Mbeya kwenda jijini Dar es Salam.

 

 

Wankyo alisema katika mahojiano ya awali raia hao wa kigeni wanadaiwa kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya biashara za kuuza baa na kusuka.

 

 

Katika tukio lingine Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Mhina Mrisho (42), mkazi wa Miono Wilaya ya Bagamoyo, kwa tuhuma za kumjeruhi kwa risasi Tatu Bakari (55), mkazi wa Miono.

 

 

Kamanda Wankyo alisema tukio hilo lilitokea Februari juzi, asubuhi, ambapo Tatu alijeruhiwa kwa kupigwa na risasi katika mguu wake wa kulia na mtuhumiwa Mhina akiwa shambani kwake.

 

 

Wankyo alisema baada ya mtuhumiwa kukamatwa alipopekuliwa alikutwa akiwa na bunduki mbili aina ya gobore, ambazo anamiliki kinyume cha sheria.

 

 

Kamanda Wankyo ametoa rai kwa watu wanaomiliki silaha pasipokuwa na vibali kuzisalimisha kwenye vituo vya polisi kwa hiari ndani ya siku saba kabla hawajakamatwa.

 

 

Aidha, alitoa wito kwa madereva na wananchi wenye tabia ya kusafirisha wahamiaji haramu kuacha biashara hiyo, badala yake watafute kazi nyingine.

Leave A Reply