The House of Favourite Newspapers

Mbatia Apata Ajali Usiku, Avunjika Mkono

MBUNGE wa Vunjo kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya kupata ajali na kuvunjika mkono jana Jumanne, Desemba 19,2017.

Mbunge huyo, amevunjika mkono wa kushoto baada ya kuteleza na kuanguka na amelazwa katika wodi za watu mashuhuri (VIP). Msaidizi wa mbunge huyo, Hamis Hamis amesema leo kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 2:45 usiku wakati akiondoka hotelini kurejea nyumbani.

Hamis amesema Mbatia alikuwa akishuka ngazi katika hoteli ya Uhuru iliyopo eneo la Shanty Town ndipo akateleza na kuanguka kisha kuumia.

“Pale kulikuwa na daktari wa KCMC anaitwa Ansbert Sweetbert ndiye alitoa huduma ya kwanza hadi kumpeleka KCMC. Dokta Ansbert alikuwa msaada mkubwa. Ndiye aliyempeleka KCMC na alikaa naye hadi saa nane usiku. Wauguzi na madaktari KCMC walimpa msaada mkubwa,” alisema Mbatia.

Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi amesema bado maumivu aliyonayo ni makali kutokana na kuvunjika mkono.

“Bado nina maumivu makali. Nashukuru sana Mungu na jopo la madaktari limeshakutana na watafanya uamuzi,” amesema.

Mbatia amesema alishapatiwa matibabu ya mwanzo baada ya vipimo vya X-Ray kuthibitisha amevunjika mkono, lakini madaktari wanafanya tathmini ni huduma gani zaidi apewe.

Comments are closed.