The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji Simba Afunguka Sababu za Kumtema Mkude

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji, amefunguka chanzo cha kiungo wake mkabaji, Jonas Mkude kutokuwemo kwenye mechi dhidi ya Coastal Union ni kutokana na kuchelewa kurudi kambini.

 

 

Sven ameongeza kwamba, Mkude alikuwa anatumikia adhabu ya kuchelewa kujiunga kambini baada ya kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa, Taifa Stars ndiyo maana hakumjumuisha kwenye msafara ulioenda Arusha.

 

 

Kiungo huyo juzi Jumamosi hakuwa kwenye kikosi cha Simba kilichopambana na Coastal Union kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo. Nyota wengine wa Simba ambao waliikosa mechi hiyo ni Luis Miquissone na Meddie Kagere waliochelewa kutoka kwenye timu zao za taifa, Chris Mugalu na Gerson Fraga wenye majeraha.

 

 

Sven amesema: “Mkude alichelewa kurudi kambini baada ya kutoka kwenye timu ya taifa, wakati wenzake wakiwa wamerejea kwa wakati sahihi. “Kwa hiyo kwenye mechi na Coastal, alikuwa na adhabu ya kinidhamu ya kuukosa mchezo huu kutokana na suala hilo la nidhamu ambalo amelifanya.”

SAID ALLY, Dar es Salaam

Leave A Reply