The House of Favourite Newspapers

Mbeya: Mwanafunzi wa Sekondari Akamatwa na Kete za Dawa za Kulevya

MBEYA: Wakati vita dhidi ya madawa ya kulevya ikiendelea Dar, imetua pia jijini Mbeya baada ya polisi kutangaza kumkamata mwanafunzi anayesoma sekondari akiwa na kete za cocaine eneo la Mbalizi jijini humo.

Kamanda wa polisi mkoa, Dhahir Kidavashari amesema Jumanne hii kuwa polisi wamemkamata mwanafunzi huyo akiwa anaziuza dawa hizo kwa watu mbalimbali na kwamba upelelezi wa kuwadaka mapapa unaendelea.

Kukamatwa kwa kijana huyo kunatokea siku moja baada ya Rais John Magufuli kuunga mkono kazi ya Makonda huku akiwaagiza wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwashughulikia wote wanaojihusisha na dawa za kulevya bila kujali huyu ni nani.

Kidavashari amesema kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya ilikuwa ikiendelea, lakini sasa imepata msukumo mpya ambao unalenga kuukata mnyororo mzima wa mtandao unasambaza dawa hizo.

Mapema Jumatatu hii Rais Magufuli alimuunga mkono Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na jitihada zake dhidi ya biashara hiyo haramu huku akiagiza jeshi la polisi kuwashughulikia wale wote wanaojihusisha na madawa ya kulevya bila kujali wadhifa wao.

Comments are closed.