Mbowe Akimbilia Mahakamani Kuinusuru nyumba Ya Mtoto Wake!
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amekimbilia Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kuinusuru nyumba iliyokamatwa kwa amri ya Mahakama ili kulipa Sh milioni 62.7 za mishahara ya waandishi wa habari 10 wanaomdai mtoto wake, Dudley Mbowe ambaye ni Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima.
Kupitia Wakili wake John Mallya, Mbowe amewasilisha shauri hilo chini ya hati ya dharura mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mary Mrio.
Leo Machi 7, 2024 Mbowe kafungua shauri dhidi ya Maregesi Paul, Fidelis Felix, Christina Mwakangale, Janeth Josiah, Exuperius Kachenje, Hellen Sisya, Kulwa Mzee, Nora Damian, Makuburi Ally, Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania News Paoer pamoja na Kampuni ya Udalali ya JJ Auctioneers & Debt Collectors.
Wakili Mallya alidai wajibu maombi tayari wamepewa madai yao pamoja na hati ya kiapo iliyoapwa na mteja wake, Mbowe Februari 26 mwaka huu.
“Mheshimiwa wajibu maombi tumeshawapa nakala hivi karibuni tusikilize kama wamekuja na majibu,”alidai Mallya.
Akijibu hoja hizo, mmoja wa wajibu maombi, Kulwa Mzee, alidai ni kweli wamepokea nyaraka hizo, zikiwa zimeambatanishwa na hati ya kiapo iliyoapwa na Mbowe, akiomba nyumba iachiliwe na Mahakama itoe amri wajibu maombi wamlipe gharama kutokana na utekelezaji wa amri hiyo ya Mahakama.
“Mheshimiwa tumepitia nyaraka wenzetu wametupa siku 15 tujibu, tunaihakikishia Mahakama kwamba tutajibu ndani ya muda tuliopewa,”alidai Kulwa.
Wakili Mallya aliomba kujibu hoja hiyo, alidai shauri lao wameliwasilisha chini ya hati ya dharura na maombi yao ni kuiondoa nyumba hiyo kwani tayari ilishabandikwa matangazo kwa ajili ya kupigwa mnada.
Alidai ikiendelea kuwa kama ilivyo inaweza kupigwa mnada kwa sababu suala hilo lina muda wa utekelezaji.
Akijibu hoja hiyo, Kulwa alidai ni kweli maombi yako katika hati ya dharura lakini lazima wasome vizuri ili wajibu kwa kuwasilisha hati ya kiapo kinzani kwa sababu katika maombi hayo kuna suala la kumlipa mwombaji gharama.
Kulwa aliomba kama siku 15 ni nyingi watajibu ndani ya siku saba, Mahakama ilikubali majibu yawasilishwe mapema; shauri hilo litasikilizwa Machi 12 mwaka huu.