The House of Favourite Newspapers

MBOWE, Wenzake Wasota Sentro 5, Waachiwa kwa Dhamana -Video

 
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wengine watano wa chama hicho wameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa takribani saa tano tangu mchana.
 
Viongozi hao walifika kituoni hapo leo Jumanne Februari 27, 2018 kuitikia wito wa polisi ili kuhojiwa kutokana na maandamano waliofanya Feb 16, mwaka huu ambapo wameachiwa saa moja usiku,
Wakili wa viongozi hao, Frederick Kihwelo amesema wote wameachiwa kwa dhamana kwa kutakiwa kuwa na mdhamini mmoja na wataripoti tena kituoni hapo Machi 5, 2018 saa moja asubuhi huku akieleza walianza kuhojiwa saa 8:30 mchana.
Februari 20, 2018 Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam liliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo Mbowe ambapo wito huo ulikuja siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo kwa mawakala wao.

 

Wengine waliohojiwa ni  Naibu Makatibu Wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni Mweka Hazina wa Bawacha huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji  akishindwa kujumuika na wenzake kwa kuwa yupo nje ya nchi kikazi.

MSIKIE WAKILI AKIFUNGUKA BAADA YA VIONGOZI HAO KUACHIWA

Comments are closed.