The House of Favourite Newspapers

Mbunge Aibua Hoja Upungufu wa Nguvu za Kiume

0

KUTOKANA  na wanaume wengi kuwa na matatizo ya nguvu za kiume, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema),Susan Lyimo,  ameishauri serikali kutoa elimu ya sababu ya baadhi ya wanaume kutokuwa na mbegu zenye nguvu ili kunusuru ndoa.

 

Susan ametoa ushauri huo wakati kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ilipokuwa ikipokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli zake jana Jumatatu Januari 20, 2020.

“Kwa kweli ndoa nyingi sana zinavunjika. Na ndoa hizi zinavunjika kwa sababu ya watu kutopata watoto, tatizo hili lilikuwapo lakini linaongezeka,” alisema.

Alisema kwa sababu ya mfumo dume walikuwa wanasema mwanamke ndiye mwenye tatizo,  lakini sasa tatizo hilo limegeuka kwa wanaume.

“Wanaume nao wakubali kwa sababu nao wana tatizo. Mimi nilikuwa nadhani kuna haja ya kutoa elimu tuone nini sababu za wanaume kutokuwa na mbegu zisizokuwa na nguvu ili wake zao ama wanawake zao wapate watoto,” amesema.

Amesisitiza  kwamba wakienda kupima vinasaba watakuta watoto wengi sana baba zao si wale wanaowajua  kwa sababu baada ya mwanamke kuambiwa kuwa hazai anaamua kuchepuka ili apate mtoto.

“Kuna haja ya kutoa elimu ili kuhakikisha tunanusuru hizi ndoa kwa sababu mimi kama mshauri naletewa matatizo makubwa zaidi. Wanawake wanajinusuru kuogopa kupewa talaka,” alisema mbunge huyo ambaye ni waziri kivuli wa elimu, sayansi na teknolojia

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii , Wazee na Watoto, Dkt.  Faustine Ndungulile,  alisema changamoto ni kubwa sana na kwamba Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam imeanza maandalizi ya kutoka huduma ya ugumba.

“Tafiti duniani zinaonyesha kuwa kwa miaka 50 kumekuwa na upungufu wa asilimia 50 ya nguvu za kiume. Nilikuwa nasoma tafiti moja inasema katika miaka 50 ijayo basi wanaume wote hapa tutakuwa hamna kitu,” alisema.

Alitaja visababishi kuwa ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, aina ya maisha na vyakula. Hata hivyo, Ndungulile alisema si kweli watoto wengi wanabambikiwa baba kwa sababu wanaokwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ni wale wenye hofu vya kuwa watoto si wao.

Alisema hata wale wenye hofu na kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupima ni chini ya asilimia 50 ndiyo wanagundua kuwa wamebambikiziwa watoto.

Chanzo: Mwananchi

Leave A Reply