The House of Favourite Newspapers

Vanessa Ale Bata, Asisahau Muziki!

0

PENZI jipya lina raha yake wewe! Unaweza ukasahau hata kula au kuwaona na kuwasalimia wazazi wako kwa sababu tu unafurahia uhusiano mpya ulioupata na ukakushika vilivyo.  Kila anayefuatilia burudani ndani na nje ya Bongo, anajua jinsi staa wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee a.k.a Vee-Money anavyofurahia uhusiano wake wa kimapenzi na staa wa Marekani mwenye asili ya Nigeria, Olurotimi Akinosho ‘Rotimi’.

Ndiyo! Vanessa anakula bata la hatari kwenye ardhi ya Rais Donald Trump baada ya kuachana na aliyekuwa mpenzi wake wa muda mrefu ambaye naye ni staa wa RnB Bongo, Juma Mussa ‘Jux’.

Penzi la Vanessa na Rotimi ambaye ni staa wa muziki, modo na mwigizaji wa Tamthiliya ya Power, linaonekana kuwa na afya ya kutosha. Tangu Vanessa awe kwenye uhusiano na Rotimi, muda mwingi anakuwa kwa mpenzi wake Marekani kabla ya juzikati wote kutinga Bongo.

Tangu Vanessa amekuwa na Rotimi, hasikiki sana kwenye muziki. Amekuwa kimya, tofauti na zamani. Kinachozungumzwa juu ya Vanessa kwa sasa ni kuhusiana na penzi lake hilo kuliko kazi yake ya muziki.

Nimeamua kuandika makala hii kwa ajili ya kumshauri Vanessa kwamba mapenzi yasimsahaulishe kazi yake ya muziki kwani yapo tu na yataendelea kuwepo siku zote.

Atakaposahau kazi yake ya muziki, atarudi nyuma na kusahaulika kwenye ulimwengu huo kwa sababu kila kukicha wanaibuka wanamuziki wapya, tena wanaofanya vizuri mno.

Vanessa asiruhusu mapenzi yakamuharibia kazi yake ambayo ndiyo imemtambulisha hadi huyo Rotimi akamuona na kumfahamu kwani kama angekuwa mkulima tu na siyo mtu maarufu, ingekuwa vigumu kumuona na kuanzisha naye mapenzi.

Kutokana na nafasi hiyo aliyoipata Vanessa, anatakiwa kuitumia vizuri kikazi; yaani kumtumia Rotimi kuutangaza muziki wake kimataifa zaidi na zaidi kwa sababu kwa hapa Bongo, Vanessa ni kati ya wanamuziki wa kike wanaofanya vizuri kwenye Bongo Fleva.

Vanessa ana mashabiki wengi na Watanzania wengi wanampenda, ishu za kuachia picha zikimuonesha akiwa na mpenzi wake maeneo mbalimbali; mara Marekani, mara Dubai na kwingineko siyo mbaya ni vizuri, lakini asiendekeze bata kwa sababu mwishoni atakuja kujutia.

Kuna mifano ya mastaa wengi ambao wamewahi kuwa kwenye mapenzi na kuonekana wakila bata sehemu mbalimbali duniani, lakini mwishoni walimwagana na kila mmoja akaendelea na maisha yake japokuwa siliombei hilo kwa Vanessa.

Tahadhari ni nzuri kabla hatari haijatokea, hivyo Vanessa cha kufanya anatakiwa kuwa na tahadhari ya kuendelea kufanya kazi za muziki kama zamani, tena ikiwezekana iwe zaidi ya hapo ili hata siku ikitokea bahati mbaya wakamwagana, basi awe na kitu cha kujivunia kuwa alikuwa kwenye uhusiano na mtu wa nje ya Bongo na akaweza kutangaza kazi zake kimataifa.

Asikubali kuja kujuta baadaye, ni vyema akashtuka mapema na muda mwingi awaze kazi yake na kwamba Watanzania wanataka kusikia kazi mpya kutoka kwake. Akishafanya hivyo, aendelee kujiachia na mpenzi wake kama kawaida.

Wapo wanaodai kwamba Vanessa amekuwa akijiachia na mpenzi wake viwanja tofauti na kupiga picha za kimahaba kisha kuposti mitandaoni kwa kuwa anataka kumrusha roho aliyekuwa mpenzi wake Jux, yaani anamlipizia kwa kuwa na yeye alifanya hivyo wakati alipoingia kwenye uhusiano na mrembo kutoka Thailand; Nayika Thongom.

Kama maneno haya yana ukweli, Vanessa anatakiwa kubadilika na kuacha mara moja kwani siku zote mapenzi siyo mashindano, unapokuwa kwenye uhusiano, ishi wewe kama wewe, usiishi kwa kumkomoa mtu.

MAKALA: GLADNESS MALLYA

Leave A Reply