The House of Favourite Newspapers

Mbunge Peneza Aanika Mbinu Wanawake Kufanikiwa!

MAFANIKIO yamemaanishwa kwa kila mwenye bidii. Leo kwenye safu hii ya Ulipo Mwanamke Tupo (UMT), tunaye Mbunge wa Viti Maalum akiwakilisha mkoa wa Geita kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Upendo Furaha Peneza ambaye ameeleza mengi sana kuhusu maisha na neno la faraja kwa wanawake, tumsikilize.

UMT: Umezaliwa lini na umekulia kwenye familia ya aina gani?

Upendo: Nimezaliwa mwaka 1988, nimekulia kwenye familia ya kipato cha kati ambapo baba akiwa daktari na mama ni mwalimu.

UMT: Kwa hiyo umekulia na kusomea Geita? Una elimu gani?

Upendo: Nimesomea maeneo tofautitofauti, ikiwemo Uganda, Arusha na Dar es Salaam. Kuhusu elimu yangu nina shahada ya Ustawi wa Jamii (Sociology).

UMT: Nje ya siasa unafanya kazi gani nyingine?

Upendo: Mimi ni mkulima. Nalima korosho na mazao mengine ya chakula.

Katika maisha kamwe huwezi kutegemea mlango mmoja kujiingizia kipato na mimi siko kwenye ubunge kwa sababu ya kipato, nilichagua siasa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na moyo wangu unafurahia sana kufanya hivyo, nalala na kuamka nikiwaza mahitaji ya wananchi wa Mkoa wa Geita.

UMT: Unawezaje kugawanya muda wa kusimamia kilimo na kuwatumikia wananchi?

Upendo: It’s all about awareness (ni suala la ufahamu tu) kwamba nini kinatakiwa kifanyike wapi na kwa wakati gani.

Ukilijua hilo kila kitu kwako kitaenda sawa.

UMT: Ni kazi gani kubwa ambayo umekuwa ukiipigania kama mbunge mkoani Geita?

Upendo: Vijana kupewa haki katika uchimbaji wa madini lakini pia nimekuwa mstari wa mbele kupigania ustawi wa elimu hususan kwa watoto wa kike, ndiyo maana nimejiandaa kuwasilisha hoja binafsi bungeni kushinikiza wasichana wapewe Sanitary Pads (pedi), shule zote kwa ngazi za msingi na sekondari.

UMT: Unawakilisha Geita na sasa uko Dar, unawezaje kuwatumikia wananchi wako?

Upendo: Naishi Geita. Maisha yangu yote ni huko na sehemu ninayoishi inaitwa Katoma. Nje ya Geita ni Dodoma bungeni huku Dar ni kwa mahitaji binafsi tu, lakini huwezi kunikuta Dar kwa zaidi ya siku tatu au wiki nzima, hilo hakuna. Naipenda sana Geita.

UMT: Ili mwanamke atimize ndoto zake ni mambo gani muhimu anapaswa kuyafanya?

Upendo: (akimkazia macho mwandishi) Is to get focused (ni kuwa na malengo), kuanza mapema, kuwa na juhudi zisizokuwa za kawaida, kuheshimu uamuzi na kumtegemea Mungu. Unajua Mungu ametuumba kila mtu na kusudi lake.

Huyu amemaanishwa kufanya biashara, yule kufundisha, fulani yeye ni ufugaji na kuna waliopangiwa kuhubiri neno la Mungu, kwa hiyo kila mmoja na ajichunguze anaweza kufanya nini na hapohapo achukue hatua (anaendelea)…

Waingereza wana msemo wao mzuri sana huwa napenda kuutumia. Wanasema: “To get what you want, you must first decide what you want and knowing what you want is the first step towards getting it.”

Kiswahili: Ili upate unachokitaka ni lazima kwanza uamue unachokitaka na kujua unachokitaka ni hatua ya kwanza kuelekea kukipata. (anaendelea)…

Maisha jamani ni namna ambavyo mtu unaamua yawe. Matatizo na changamoto zipo lakini ishu siyo tatizo, bali muhimu ni namna gani unalitazama tatizo lenyewe. Ukiliona tatizo ni kubwa kweli linakuwa kubwa lakini kama ukilipuuza na kujikita kwenye kulitatua, maisha yatakuwa mepesi sana.

UMT: Upendo Peneza nikushukuru kwa muda wako na maarifa yako, endelea kuwatumikia wananchi wa Geita.

Upendo: Barikiwa na Mungu, karibu tena na endelea kupigania ndoto zako.

 

Makala: Brighton Masalu, ULIPO MWANAMKE

Maoni, ushauri: 0673-423 845 TUPO

Comments are closed.