MCHAWI WA DEREVA BREKI

SHOGAAAAA eeehh wanak-wambia hata kizibo ni mfuniko japokuwa huwezi kufunikia sufuria, heee heeeeiyaaaa! Tangu lini kijiko cha jikoni kikaogopa moto? Unajifanya mjanja wa mjini wakati simu yako ina MB 4, haloooo eeeeh! Endelea tu na tabia yako, umesahau kama mwanamke wa baa hatongozwi asubuhi! Shoga hakuna kitu kinanikera kama mtu kujifanya maji ya nazi anataka kuyapikia kwenye chai. Ndiyo maana wala sishangai ndoa nyingi za vijana wa sasa zikidumu sana basi mwaka au miezi mitano kama siyo sita.

Kila siku natumiwa malalamiko hadi nachoka, ukija kuuliza miaka yake anakwambia 20 hata kicheni pati tu hakufanyiwa unafikiri atadumu na mwanaume huyo? Shoga mapenzi siyo kukurupuka, hata ndoa siyo leo mmeonana sijui umeona kama ana sifa unazozihitaji hapohapo ndoa unawekwa ndani bila kujua kesho na keshokutwa akikuona gogo anaona mwingine, upo nyonyo?

Kungwi mwenyewe niliyepitia mishale mingi nimekuwa nikitoa ushauri kwa mabinti zangu wengi, jamani hata kama wewe mmojawapo unasoma hapa, kabla ya kuolewa basi uwe na angalau akili ya kwenda kuishi kwa mwanaume, utoto wa kuchati na simu, magrupu karibu 20 mwanaume akienda kazini upo na simu akirudi upo na simu si bora uwe mhudumu wa mtandao wa simu tu!

Kama ulikuwa hujui ngoja nikung’ate sikio shoga! Mchawi wa dereva ni breki tu hakuna kingine! Mwanamke unatakiwa uwe kama dereva ufundwe ukafundika, ujue kupika jikoni na kupika chumbani siyo hata kusugua sufuria huwezi! Unatakiwa ujue maneno yote ya kumwambia mumeo iwe jikoni, sebuleni au chumbani upo nyonyo?

Sawa umeolewa na umri mdogo na pengine hata hiyo kicheni pati hukupitia basi watafutwe makungwi wakakuonyoosha! Wakakupa mbinu zote za kuishi na mumeo! Ujue mumeo akiwa na hasira unatakiwa umkabili vipi, wengine hata kupanga tu uzazi wa mpango hawajui! Shoga nisiwe muongeaji sana nikajikuta mengine naropoka, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi. Ni mimi Anti Naa Shangingi Mstaafu

Toa comment