The House of Favourite Newspapers

Mchawi wa Yanga ni Huyu Hapa

0

LICHA ya usajili wa gharama kubwa ambao wameufanya Yanga ikiwemo kwenye eneo la ulinzi, lakini mashabiki wa timu hiyo hawana furaha na kikosi chao kutokana na matokeo mabaya wanayoendelea kuyapata.

 

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu Mtunisia, Nassredine Nabi, Jumapili katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali, waliendelea na mfululizo wa matokeo mabaya baada ya kufungwa na Rivers United ya Nigeria kwa bao 1-0.

 

Mchezo huo ni wa pili kwa Yanga kupoteza mbele ya timu ya nje ya Tanzania baada ya awali kufungwa mabao 2-1 na Zanaco FC ya Zambia.

 

Wakati wengi wakitafuta chanzo cha Yanga kufanya vibaya katika mechi zake, Spoti Xtra limekaa chini na kuchunguza kwa umakini kile ambacho kinaigharimu timu hiyo na kuleta majibu yafuatayo.

 

Shida kubwa ambayo Spoti Xtra imegundua kwenye kikosi cha Yanga ni wachezaji wake kutokuwa vizuri katika kuokoa hatari wakati wa mipira ya kutengwa.

 

Hilo lilijidhihirisha wazi Jumapili kwenye mechi dhidi ya Rivers United ambapo bao pekee lililofungwa dakika ya 51 na Moses Omoduemuke, lilitokana na tatizo hilo.

 

Bao hilo lilipatikana baada ya mpira wa kona fupi iliyoanza na Rivers United, kabla ya kupigwa krosi ambayo iliunganishwa kwa kichwa na kumkuta mfungaji aliyemalizia kwa kichwa pia huku walinzi wa Yanga wakishindwa kujipanga vema kuokoa hatari hiyo.

 

Ukitazama mchakato wa bao ulivyoanza hadi linapatikana, tatizo lilianzia kwa Yacouba Songne ambaye aliona pigo la kona fupi, lakini hakukaba hadi mwisho ambapo mpinzani wake alipiga krosi na kuzaa bao.

 

Pia ndani ya boksi la Yanga wakati bao hilo linafungwa, kulikuwa na wachezaji nane wa timu hiyo, huku wapinzani wakiwa watano pekee.

 

Achana na bao hilo, wakati Yanga inafungwa 2-1 na Zanaco, mabao yote mawili yalitokana na staili kama hiyo ya mipira iliyokufa, huku wapinzani wakianzishiana pasi fupifupi.

 

Katika mechi hiyo, bao la kwanza la Wazambia hao ambalo lilifungwa na Achim Mumba, lilitokea baada ya mpira wa kona ambao ulipigwa, beki wa Yanga, Djuma Shaaban katika harakati za kuokoa, akaupiga mpira kichwa cha nyuma na kumkuta mfungaji akiwa mwenyewe na kuukamishwa mpira kimiani kirahisi.

 

Bao hilo pia ilikuwa ni kushindwa kukaba nafasi kwa wachezaji wa Yanga lakini pia kushindwa kumkaba mtu. Wakati bao likifungwa, Yanga walikuwa na wachezaji tisa kwenye boksi lao, huku Zanaco wakiwepo sita.

 

Lile bao la pili lililofungwa na Kapumbu, Zanaco walianzisha mpira wa kurusha karibu na eneo la hatai la Yanga, zikapigwa pasi tatu za haraka, akatafutwa mfungaji ambaye hakuwa amekabwa, akaukwamisha mpira kimiani huku wachezaji nane wa Yanga wakiwa karibu na eneo hilo wakishindwa kufanya jambo lolote.

 

Safu ya ulinzi ya Yanga msimu huu ipo hivi; Kibwana Shomary, Paul Godfrey, Djuma Shaban, David Bryson, Adeyum Salehe, Yasin Mustapha, Abdallah Shaibu, Yanick Bangala Litombo, Bakari Mwamnyeto na Dickson Job.

 

Akizungumzia bao walilofungwa Yanga Jumapili, mchambuzi na kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Mayay, alisema: “Kulikuwa hakuna umakini katika kuokoa ile hatari, tazama namna walinzi wa Yanga walivyojipanga, waliwaacha wachezaji wa Rivers wakiwa huru.

 

“Wanapaswa kuwa makini kwenye mipira hii iliyokufa kwani inaonekana kuwa hatari zaidi kwao, msimu huu wasipokuwa makini wanaweza kuruhusu mabao mengi. Kocha anapaswa kufanya kitu.”

Mwandishi Wetu

Leave A Reply