The House of Favourite Newspapers

Mchezaji wa Yanga hali tete

0

INATISHA! Hali ya mchezaji wa zamani wa Yanga, Nsa Job ni tete inayohitaji maombi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi kufuatia kupigwa jiwe kichwani katika vurugu za uchaguzi mkuu zinazoendelea katika kampeni zinazofanyika Moshi Mjini, Ijumaa linakuhabarisha.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Coastal Union (kulia).

Nsa ambaye pia amewahi kuzichezea timu za Moro United, Simba na Coastal Union alikuwa njiani akitokea nyumbani kwa mgombea ubunge wa jimbo la Moshi mjini kupitia CCM, Davis Mosha alipopigwa jiwe lililovunja kioo cha gari alilopanda na watu wanaosadikika kuwa ni wafuasi wa Chadema.

Jiwe hilo lilimpiga kichwani kitendo kilichosababisha mchezaji huyo kupoteza fahamu na sasa hali yake ni mbaya akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) ambako madaktari wanapambana kuokoa maisha yake.

Mosha aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga wakati Nsa akiwa mchezaji katika kikosi cha timu hiyo.

“Hii siyo siasa, huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine, tunaomba vyombo vinavyohusika vifanye kazi yake ili mambo haya yasiendelee. Haiwezekani watu tukafikia hatua hii ya kufanyiana unyama huu halafu tunasingizia siasa. Na kama siasa zenyewe ndiyo hizi, basi taifa linahitaji maombi maana hali ni mbaya,” alisema mwananchi mmoja aliyedai kumuona Nsa akiwa hoi hospitalini hapo.

Shuhuda wa gazeti hili aliyeko mjini Moshi, alisema hali ya usalama imekuwa tete miongoni mwa wafuasi wa vyama hivyo vyenye upinzani mkali kwa sasa kutokana na matukio ya vurugu kutokea mara kwa mara katika baadhi ya maeneo ya kampeni.

Wakazi wa Moshi wataungana na Watanzania wengine kote nchini keshokutwa katika kupiga kura ya kuchagua rais, wabunge na madiwani katika uchaguzi ambao viongozi mbalimbali wa dini wametaka amani itawale.

Leave A Reply