The House of Favourite Newspapers

Mchungaji wa Kutetema…. Viongozi wa Dini Wapongeza Serikali

SIKU chache baada ya Serikali kupiga marufuku ibada zinazoendeshwa na kiongozi wa kanisa la Mfalme Zumaridi lililoko mtaa wa Iseni Kata ya Butimba, jijini Mwanza, baadhi ya viongozi wa dini wameipongeza Serikali na kuiomba ifanye uchunguzi zaidi kwa makanisa mengine.

 

Mchungaji wa kanisa hilo aliyevuma kwa jina la ‘Mchungaji wa Kutetema’ kutokana na staili yake ya kutetemeka anapoingia kwenye ibada, limefungiwa kutokana na madai ya kuhatarisha usalama wa waumini na kukinzana na sheria za nchi.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki chache zimepita baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela kueleza kushangazwa na mhubiri Zumaridi na kuhoji sababu za kiongozi huyo wa dini kujiita Mungu.

 

VIONGOZI WAKEMEA

Wakizungumza na Amani kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi wa dini walisema asilimia 90 ya makanisa hayo ya kiroho yanatakiwa kuchunguzwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Viongozi wa Dini, Askofu William Mwamalanga, aliipongeza Serikali kwa kuchukua hatua haraka kuhusu kanisa hilo, na kutoa wito kwa Watanzania kuwa macho ili kuwatambua wachungaji wa uongo.

 

Alisema kamati anayoiongoza, ilikwenda Mwanza baada ya kupata malalamiko kwa wachungaji wa mkoa huo ambao walifuatilia mahubiri ya kanisa hilo la Zumaridi, na kubaini linakwenda kinyume na taratibu na tamaduni.

 

“Kamati ya ulinzi na usalama imefanya jambo jema, kwa sababu ilibaini pia huyu mchungaji wala hana hata ushirikiano na wachungaji wenzake…alikuwa anaficha kila jambo analofanya. Wakati suala la Mungu lipo wazi, ni peupe hakuna kufichaficha,” alisema.

 

Alisema kiuhalisia utaratibu wa ukristu una mpango wa Mungu kwelikweli ndio maana wachungaji wa uongo wakiingiza makandokando yao wanaumbuka.

“Tulikuja kugundua anachofanya siyo mambo ya kimungu, hivyo Serikali imeungana na kamati yetu. Huwezi kusema wanadamu walale chini upite juu yao, au wale udongo ili wapate utajiri!

 

“Napenda niwaonye Watanzania mafundisho ya uongo ni mengi, wasiwe na haraka ya kutafuta mali, kazi za kupata mali zipo na Mungu ametubariki kupitia mikono yetu…sio kwa kuambiwa kula udongo au kinyesi ni aibu sana,” alisema.

 

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mchungaji wa Kanisa la Maombezi GRC la jijini Dar es salaam, Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako, ambaye pia aliipongeza Serikali kwa kulifunga kanisa hilo.

Aidha, aliiomba Serikali iendelee kufanya uchunguzi zaidi kwa sababu asilimia 90 ya makanisa hayo ya kiroho ni feki.

 

“Yaani nawapongeza sana, kwa sababu siku hizi kuna mambo ya ajabu sana, mtu anajiita mtume, wakati mtume wa mwisho alikuwa Muhamad, au anajiita nabii, huwezi kujiita nabii! Unabii utaonekana wenyewe, ndio maana hata Yesu alipokuja watu walikuwa wanajiuliza huyu ndiye? Alipojidhihirisha ndipo wakamgundua yeye ni nani,” alisema.

 

Hivi karibuni Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospal Bible Felllowship Church, Zachary Kakobe pia alionya uwapo wa makanisa hayo yasiyozingatia weledi na mafundisho kweli ya kimungu.

Naye Askofu Sylvester Gamanywa aliwahi kukemea wachungaji au manabii wanaopotosha watu na kuonya watu kuwa makini.

 

AGIZO LILIVYOTOLEWA

Agizo la kupiga marufuku lilitolewa mapema wiki hii na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Dk. Philis Nyimbi akiwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo katika eneo la kanisa hilo.

 

Dk. Nyimbi alisema kanisa hilo limekuwa likitumia katiba ya kanisa lingine ambalo ni Pentecoste Christian Church of Tanzania na pia limekuwa likitembea na katiba ya kanisa hilo.

 

Sababu ya tatu, ilielezwa kuwa Mfalme Zumaridi amekuwa akiendesha kanisa hilo bila kufuata sheria za nchi wala maandiko matakatifu kwa kujiita Mungu wa Dunia, Mfalme wakati yeye ni mwanamke.

Stori: Gabriel Mushi, Dar

Comments are closed.