Mdomo Hauna Vocha

WAREEEEREEE shoga yangu najua umezoea cheko la nyundo haya sasa leo nakupa la msumari nginja nginja! Haya tena sikukuu ndiyo hiyoo imepita kaama hukushiba kwa tonge basi kaa ukijua huwezi kushiba hata kwa kujilamba, upo nyonyo? 

 

Wajanja wa mjini wanakwambia raha ya kuringa upate wa kumringia siyo umetoa macho unashindwa kuelewa kama muwasho wa ulimi haukunwi kwa vidole!  Hee heeeiya mdomo komaa nani aliyekudanganya honi inafungua geti?

 

Shoga leo nimetua zaidi ya maji ya mtungini! Mji mzito huu yaani kila ukitatua hili linakuja lingine utafikiri wakunga kama siye hatuzeekagi! Sawa nakubali kuwa mbuzi miye yangu kamba mnyororo utaniumiza!

 

Hebu tung`atane sikio mwenzangu maana hili nalo limekuwa janga kila leo wanawake wenzangu wamekuwa wakinilalamikia nikashusha maji kwenye koo nikasema siwezi kuwa kama majani ya chai hayajulikani kama ni tiba ya ngiri au kichwa! Halooooo eeeeehh!

Shoga heri karipio la rafiki kuliko busu la mnafiki na ukimuona mwanamke mzima anaomba msaada ujue limemshika hiloo! Basi kuna mwanamke mwenzetu kanikumbusha jambo ambalo nimeamka nalo leo nikasema siwezi kuliacha lielee juujuu kama maji ya mtungini yasiyotabirika na ubaridi wake.

 

Shoga yangu ananiambia amekuwa akijisikia vibaya namna mumewe anavyokuwa karibu na simu yake ya mkononi kuliko mapenzi. Yaani inafikia kipindi akitoka kazini ni kuchati muda wote mbaya zaidi mwanaume huyo hamuoneshi simu yake kaipiga loki kila kona utafikiri bomba la maji la kulipia!

 

Nikahoji si ujaribu kumuibia akiwa amelala halafu uchunguze kwenye meseji hadi utamjua mbaya wako! Wapi shoga! Hizo loki alizoweka zimeenda shule hadi likizo!

 

Niwageukie na nyie wanaume, hivi kwanza hamjui mgonjwa hajiambukizi na bahati ya mbwa kupendwa na Mzungu! Hebu nisikilize msikilizike siyo linaingia sikio hili na kutokea lile! Mwanamke anatakiwa kuheshimiwa, mwanamke anatakiwa kuwekwa wazi utaona mapenzi yanavyokuwa rahisi!

Mdomo hauna vocha! Wanawake wengi siyo waongeaji linapotokea tatizo hasa linalomhusu yeye na mumewe au mchumba wake na hili limekuwa likituumiza sana sisi wanawake!

 

Jamani mdomo tumepewa hakuna cha kuukwangua kama vocha uweke ndiyo uongee! Washirikishe marafiki zako wa karibu au ndugu waweze kumuweka sawa mumeo siyo umenyamaza kama honi ya treni hadi ione wanyama au ikatishe katikati ya watu ndiyo ipigwe, shuuutuuuu!

 

Shoga yangu kaa utambue gogo halisukumwi kwa haja ndogo! Ukiona mwanaume wako anakosea au anapenda kujitenga na simu yake jua kuna kitu kinaendelea hataki ujue! Sasa jiulize usipojua wewe anataka nani ajue?

Kaa na mumewe muwekane sawa! Kama hizo loki anaziweka kwenye simu kwa ajili ya watoto basi uzijue namna ya kutoa na hata wewe shoga mumeo awe na uwezo wa kuchukua simu yako na kuitoa loki kama itakuwepo huo ndiyo upendo na utawafanya muaminiane!

 

Nisiwe muongeaji sana hadi mdomo wangu ukachachuka! Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Ni mimi Shangingi Mstaafu ukipenda niite Anti Nasra!


Loading...

Toa comment