The House of Favourite Newspapers

MEGHAN ALIKUBALI KUACHIKA ATIMIZE NDOTO ZAKE

Prince Harry Akiwa na Mkewe Rachel Meghan Markle.

TANGU wikiendi iliyopita, gumzo duniani kote lilikuwa harusi ya kifahari ya mjukuu wa Malkia wa Uingereza, Elizabeth II, Prince Harry, ambaye ni mtoto wa Mfalme wa Wales, Prince Charles aliyefunga ndoa na muigizaji wa zamani kutoka Marekani, Rachel Meghan Markle. Mbali na mengi yaliyovutia kwenye harusi hiyo, mambo mawili yameweza kuvunja historia baada ya wawili hao kuoana.

Kwanza kabisa, Meghan amekuwa mwanamke wa kwanza kutoka Marekani kuingia kwenye familia hiyo ya Kifalme na Malkia bila kipingamizi chochote kile. Lakini pia, jambo la pili ni historia yake, kutoka kuigiza mpaka kupata heshima hiyo aliyonayo kwa sasa duniani. Katika toleo hili, Meghan ndiye mwanamke wa chuma tuliyenaye na makala hii itakueleza mambo kadhaa ambayo ilibidi afanye ili kutimiza ndoto zake.

ALIPITIA MAISHA MAGUMU

Meghan aliyezaliwa na kukulia Los Angles, California, Marekani wakati wa ukuaji wake amepitia maisha magumu pamoja na mama yake Doria. Hiyo ilitokana na wazazi wake kuachana akiwa na umri wa miaka 6, na mama yake kulazimika kumlea akiwa peke yake.

Lakini Meghan amewahi kuweka wazi kwamba maisha magumu aliyopita hayakuweza kumkatisha tamaa katika ndoto zake za uigizaji. Alilala na kuota kuigiza, jambo ambalo aliweza kulifanikisha katika maisha yake.

HAIKUWA RAHISI KUTOBOA

Hakuna mtu aliyewahi kutimiza ndoto zake kirahisi. Kila mwenye ndoto inabidi apambane ‘kufa na kupona’ kuweza kutimiza ndoto zake.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Meghan. Mwanadada huyu alianza kutafuta mlango wa kutoka kupitia uigizaji wakati akiwa hajamaliza hata masomo yake katika Chuo Kikuu cha Nothwesten alikokuwa anasomea masomo yaliyohusu Michezo ya Kuigiza na Mafunzo ya Kimataifa.

Mungu saidia, aliweza kubahatika kupata nafasi ya kuigiza kwenye filamu ya Deal or No Deal akiwa na miaka ishirini tu. Lakini unafikiri ndiyo alikuwa ametoka? Aaah wapi! Ndiyo kwanza safari ilikuwa imeanza.

Alipitia changamoto nyingi kwani baada ya kumaliza shule kabla hajapata nafasi ya kutengeneza pesa ilimbidi kwenda kwenye ‘audition’ za kuigiza akiwa na kigari chake kibovu kilichokuwa hakifunguki kwenye upande wa mlango wa dereva, alishindwa kuutengeneza mlango huo kwani hakuwa na pesa.

Meghan alizidi kupambana mpaka akafanikiwa kupata dili za kuonekana kwenye filamu za Remember Me, Horrible Bosses, A Lot Like Love, Get Him to The Greek na Candidate. Hata hivyo amefanya ‘series’ za Fringe, The War Of Home, Knight Rider, Without a Trace na iliyomtoa na kumpa mafanikio makubwa ni Suits.

ILIBIDI AACHIKE KUTIMIZA NDOTO ZAKE

Kabla ya kuolewa na Prince Harry, Meghan mwaka 2011, aliolewa na muigizaji mwenzake ambaye ni muandaaji wa filamu pia aitwaye Trevor Engelson, aliyekuwa naye kwenye uhusiano kwa miaka sita. Lakini ‘guess what?’ Meghan hakujali kuwa kwenye uhusiano kwa muda wote huo, wala kuolewa mbele za ndoto zake.

Alipoanza kuigiza series ya Suits nchini Canada, mumewe alimchoka kutokana na umbali. Alipomueleza kuhusu kuachana hakuwa na kipingamizi, kwani aliweka wazi kuwa asingeweza kuacha ndoto zake zipotee kisa ndoa.

HAKUWA NA SKENDO

Suala hili wanaweza kujifunza waigizaji wetu nchini au mwanadada yeyote yule mwenye ndoto za kuigiza. Hivi unafahamu kwamba inawezekana kabisa kuwa muigizaji mzuri na usiwe na skendo!

Kama iliwezekana kwa Meghan, wanashindwa nini mastaa wengine hapa Bongo? Kwa taarifa yako unayesoma, ingawa mwanadada huyu hakuwa na skendo kiivyo, lakini ndiye muigizaji aliyetafutwa zaidi kwenye mtandao wa ‘Google’ mwaka 2016, lakini maisha yake ya bila skendo za ‘kipuuzi’ yameweza kumfanya kukubalika kuingia kwenye ukoo wa malkia.

MAMBO AMBAYO HAWEZI KUFANYA TENA

Furaha katika maisha ni kutimiza ndoto na mengi ambayo umekuwa ukiyaota. Ingawa mwanadada huyu hataruhusiwa kuigiza tena baada ya kuingia kwenye ukoo wa Kifalme na Malkia lakini ndoto zake ameshatimiza.

Jambo lingine ambalo haruhusiwi kufanya ni kumiliki akaunti kwenye mtandao wa kijamii wowote ule. Hakuna anayeruhusiwa katika ukoo huo na tayari Meghan ameshajitoa kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram.

Lakini pia hawezi kusaini karatasi na vitabu wala chochote kile mtaani kama ilivyokuwa zamani wakati akiwa muigizaji. Katika ukoo huo hakuna anayeruhusiwa kuepusha sahihi zao kudukuliwa.

Jambo lingine ambalo haruhusiwi ni kuonesha upande wa kisiasa. Hata Malkia Elizabeth II, haruhusiwi kufanya hivyo. Wote katika familia hiyo wanachotakiwa ni kuelekeza hisia zao za kisiasa kwenye kazi za kijamii!

Makala: Boniphace Ngumije

Comments are closed.