The House of Favourite Newspapers

Meja Jenerali Msuya; Alivyokufa na Kufufuka

0

ILIPOISHIA:
TULIBISHANA kwa hoja kwa muda kidogo kwa vile alikuwa na mawazo kwamba India ingekuwa mahali bora zaidi kwangu na kwake kutokana na bajeti iliyokuwepo. Nilisisitiza nikatibiwe Uingereza kwani niliwahi kuutembelea Ubalozi wa Tanzania huko nyuma mnamo miaka ya mwisho ya 1980, jambo ambalo lilinipa fursa ya kuwafahamu wataalam wengi bora wa magonjwa.  Kwa Upendo wa Mungu, alikubali na akafanya uamuzi huo mgumu.
ENDELEA…

Alikubali gharama zigawanywe, ambapo serikali ingelipia usafiri na gharama za matibabu na familia yangu ingegharimia malazi, chakula na usafiri wa ndani. Nilijua mpangilio huo ungefanya kazi vyema kwa vile mwanangu wa kiume alikuwa anaishi Uingereza. Hiyo ilikuwa ni baraka kutoka kwa Mungu.

Hivyo, alimwagiza Mnadhimu Mkuu, Jenerali Abraham Shimbo, kuitisha mkutano siku iliyofuata ili kuratibu mipango ya tiba yangu na masuala ya kiutawala. Shimbo alimwita Mkuu wa Tiba, Mkuu wa Hospitali ya Kijeshi, Mkuu wa Utumishi na baadhi ya maofisa husika ili kuliweka sawa suala hilo.

Mwanangu Bisala na binti yangu Annia, walikaribishwa katika mkutano huo kuelezea tatizo langu. Ugumu ukawa katika kugharamia matibabu, yaani ni katika kasma gani ambayo ingetoa fedha hiyo kwani gharama hiyo ilikuwa haikupangwa, hivyo haikuwa ndani ya bajeti.

Hatimaye, palifikiwa makubaliano na Mwambata wa Kijeshi huko London aliyeambiwa anitayarishie daktari katika Kliniki ya London.  Hilo lilinipa faraja kubwa, nilijiona kama tayari nilikuwa nimepona. Ni baada ya tukio hilo ambapo nilitambua kwa nini nilijisikia hivyo.

Nilichoking’amua ni kwamba Mungu alitaka kunionesha jinsi mipango yake ilivyokuwa inatekelezeka, mipango ya mambo ambayo ilikuja kufunguka baadaye wakati wa matibabu. Mungu pekee hufahamu mwisho wa jambo fulani tangu mwanzo wake.

Siku hiyo niliyokuwa na mkuu huyo wa majeshi (CDF),  niliondoka na kwenda moja kwa moja nyumbani badala ya kuripoti tena katika Hospitali ya Kijeshi. Mnamo alasiri, nilishikwa na homa kali iliyoambatana na kutetemeka kwa nguvu. Hivyo, Bisala alikwenda kumwita daktari kutoka hospitali ya karibu. Daktari huyo alikuja na kukaa na mimi jioni hiyo akinihudumia na akaondoka alipohakikisha kwamba homa ilikuwa imedhibitiwa.
Matokeo ya kipimo cha MRI ambayo hayakuonesha chochote, Dk. Mwanjela, aliamua kuyajumuisha katika hati ya rufaa kwa madaktari wa Uingereza.

Wakati mipango ya usafiri ilikuwa inafanywa, niliendelea kuwa karibu na madaktari ili niweze kusafiri kwenda London bila matatizo. Jamaa zangu walikuwa wananitakia heri katika safari na matibabu. Mpwa wangu, Elizabeth, alikuja nyumbani kuniombea. Katika mazungumzo yetu alinihakikishia kwamba ningepona kikamilifu kutokana na ‘kazi’ niliyokuwa naifanya katika kanisa la kijijini kwangu kama huduma kwa matakwa ya Mungu.

Alikuwa akizungumzia vigae nilivyoweka ndani ya kanisa na katika ofisi ya mchungaji, feni za kwenye dari nilizofunga kanisa zima na marekebisho kadhaa niliyofanya katika kulifanya kanisa hilo liwe mahali bora zaidi kwa ibada. Pia nilikuwa nimechangia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa ofisi za parokia ikiwa ni pamoja na ukumbi wa mikutano wa kanisa hilo.

Alipomaliza kusali, alisema alikuwa na ujumbe kutoka kwa mpwa wake Edna aliyekuwa anaishi Arusha, mji maarufu kwa utalii nchini Tanzania.  Wawili hao umri wao ni rika moja (wakiwa kwenye miaka sitini na zaidi). Ujumbe wenyewe ulikuwa ni kwamba alikuwa ameota kwamba aliniona nimerejea kutoka kwenye matibabu nchi za nje ambapo nilionekana katika afya njema na kwamba alinisindikiza hadi kwangu ambapo alinishauri niache biashara ya kugawa bia katika Wilaya ya Mwanga kwa niaba ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Wanawake hawa wawili wanamwogopa Mungu na ni wafuasi wazuri wa dini zao. Edna alibatizwa katika Kanisa la Kilutheri na ameendelea katika imani hiyo hadi leo.  Elizabeth alibadili na kujiunga na Kanisa la Assemblies of God, lakini umri ulivyozidi kusonga mbele alirejea katika Kanisa la Kilutheri.

Kwa upande wangu, dini huwa haina uhusiano wa moja kwa moja na uadilifu wa mtu. Kitu muhimu ni uhusiano wa mtu na Yesu kwani imeandikwa kwamba jina lake liko juu ya majina yote na kwamba kila goti litapigwa mbele yake na kwamba hakuna anayeweza kufika kwa Baba ila kwa kupitia Yeye. Hivyo, nini kinaweza kuwa muhimu zaidi katika ukombozi wa binadamu kuliko Yesu?  Mwenye masikio na asikie.

Safari kwenda Uingereza
Madaktari waliona nilikuwa nimepata nguvu kidogo na ningeweza kusafiri, hivyo tiketi za usafiri wa daraja la kwanza kwa ajili yangu na mke wangu zilikatwa. Nilikuwa nimependelea kusafiri na Shirika la British Airways (BA) kwa vile ingekuwa ni safari ya moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi London, bila kutua mahali. Hata hivyo, nilikuwa nimeongea na jamaa wa itifaki kuwaomba maofisa wa BA wanitayarishie kitu cha magurudumu ili kuniwezesha kupita katika kumbi ndefu zilizoko katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow.

Mambo yote yalipokamilika, nilipanda ndege ya safari namba BA46 siku ya Julai 3 ambayo iliondoka Dar es Salaam saa 2:30 asubuhi na kuwasili London saa 10:40.

Itaendelea katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.

Leave A Reply