The House of Favourite Newspapers

Sitalipa Kisasi

0

Tanzanibani Juni, 7, 2015.

KULIKUWA kumetulia mno, hakuna sauti za watu, chura wala kuku zilizosikika angani alfajiri hiyo kiasi kwamba ilikuwa vigumu kuamini kuwa kuna watu waliishi mahali hapo!
Ilikuwa ni katika eneo la Wazo, Madale, jijini Menalia umbali wa mita 1000 kutoka kilipo kiwanda kikubwa cha kusaga kokoto walikoishi watu wasio na makazi ndani ya mashimo ya kupondea kokoto walizoziuza kwa bei chee kwenye kiwanda cha jirani.

Miongoni mwa vibanda ishirini na tano vilivyokuwa ndani ya mashimo hayo kilikuwa kibanda cha Antony Malocha na mpenzi wake Matilda, wawili hao waliishi mahali hapo kuzimalizia siku za maisha yao zilizobaki duniani kutokana na kukata tamaa kufuatia mateso makubwa waliyoyapitia!

Mapito yao ilikuwa ni historia iliyomsisimua kila aliyeisikia, watu wengi walishindwa kuvumilia kuzuia machozi waliposimuliwa, kilichowasikitisha zaidi watu hao walioishi kama wapenzi kwa miaka mingi walikuwa ni ndugu wa damu kabisa, mama na baba yao alikuwa mmoja!

Tofauti na watu wengine suala hilo liliwatesa mno Antony na Matilda, walipoanzisha uhusiano wa mapenzi na baadaye kugundua kuwa ni ndugu waliokuwa wamepotezana, walijaribu mara kadhaa kuachana lakini ilishindikana.
Walikuwa wanapendana kwa dhati, Matilda alikwishajaribu mara kadhaa kujiua linapokuja suala la Antony kumuacha hasa alipotokea kupendwa na mrembo wa dunia Adelina Moshi. Jambo hilo pamoja na uvumilivu wake  ndivyo vilivyomfanya Antony kuwa tayari kufanya lolote kwa ajili ya Matilda kiasi hata cha kuvumilia kuwa naye wakati huo.

Alfajiri hiyo Antony aliamka akiwa na mawazo tele kuliko siku yoyote ile. Maisha ya kuishi kwa ‘chai na mluzi’ ndani ya kibanda alichokijenga kwa magunia na makuti yalimchosha kiasi kwamba kila siku alipiga goti kumuomba Mungu kuzinyakua roho zao kuliko kuendelea kuishi katika mateso hayo!
Pembeni ya maboksi aliyolalia na Matilda kulikuwa na kigoda kilichobeba Biblia iliyochoka na kuchanika baadhi ya kurasa zake, redio ndogo, kibatari, CD zilizochafuka kwa vumbi pamoja na bahasha ya kaki iliyochakaa ambayo ilikuwa na picha za wawili hao zilizowakumbusha machungu kila kukicha.

Antony akiwa anaendelea kuelea katika dimbwi la mawazo, aligeuza uso wake na kumtazama Matilda aliyekuwa amelala usingizi mzito. Moyo wake ulimuuma mno kutokana na jinsi mpenzi wake huyo alivyoonekana kuchoka, kuchakaa na  kufubaa kutokana na shida zilizowaandama pamoja na mateso waliyokuwa wanapitia.

Kilichomuumiza zaidi moyoni Antony ni namna ambavyo uso wa mwanamke huyo ulikuwa umeharibika kutokana na kumwagiwa tindikali na Adeline kiasi kwamba hata macho yake yaliziba kitendo kilichomsababishia kupoteza uwezo wake wa kuona.

Ukweli ni kwamba ilikuwa vigumu kuamini huyo ndiye Matilda aliyewavutia wanaume wengi na kuitingisha dunia kutokana na umbile lake la kuvutia, sura, mapozi lakini zaidi uwezo wake wa akili ambao wanasayansi walithibitisha kuwa haukuwa wa kawaida. Ulikuwa juu sana!
Antony alizidi kukumbuka jinsi alivyogombana na wanaume hao kutokana na wivu wa mapenzi, akaishia kumwaga machozi na kulia kwa kwikwi!

“Kila akukimbiliaye huambulia pumziko, kila akutegemeaye hupata msaada, lakini kwa nini sisi? Nini hasa tulikukosea mpaka tuteseke hivi? Zitoe tu roho zetu tumechoka kuteseka…” Antony aliongea kwa uchungu akimkumbatia Matilda na kumbusu kwenye paji la uso wake huku machozi yakizidi kumbubujika.

Kabla ya hayo yote kuwatokea Antony na Matilda walikuwa ni watu maarufu mno duniani.
Hakuna ambaye hakuwafahamu, Antony akiwa mwanamuziki, muigizaji na mfanyabiashara mkubwa sana aliyeiletea heshima nchi yake, Matilda alikuwa ni msomi aliyemiliki Shahada ya Usimamizi wa Biashara ya kimataifa kutoka Kituo cha Maendeleo ya Uchumi, Williams College kilichopo Massachusset nchini Marekani na cheti cha masuala ya fedha kutoka Chuo Kikuu cha Strathlyde.

Pia mwanamke huyo ‘genius’ aliwahi kufanya kazi kwenye benki kuu iliyopo nchini kwake, wizara ya fedha, mshauri mkuu wa uchumi serikalini kabla ya kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Baraza la Uchumi Duniani la World Economic Forum (WEF).  Kazi hizo ndizo zilizomtajirisha, kumpa jina na heshima kubwa duniani akiwa na umri mdogo tu wa miaka 38 tu.

Kilichowafikisha wawili hao kuwa mahali hapo walipokuwa lilikuwa ni suala zima la mapenzi! Bila kutegemea Antony alijikuta akiuza mali zake zote ili kujinusuru kifungo cha maisha kutokana na kesi za mauaji mfululizo alizoundiwa ‘kimagumashi’ na msichana mweusi tii! Mwenye roho mbaya, Adelina Moshi baada ya kukataa kumuoa.

Lakini upande wa pili, Matilda aliingia katika vita nzito na mwanamke huyo kutokana na kuwa katika uhusiano wa mapenzi na Antony suala lililoonekana kuwa kikwazo kwa Adelina kumpata.
Je, nini kitaendelea? Huu ni mwanzo tu, usikose kufuatilia wiki ijayo!

Leave A Reply