The House of Favourite Newspapers

Membe Akoleza Mjadala Urais 2020

0

HATIMAYE aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bernard Membe jana amepokelewa rasmi ndani ya Chama cha ACT Wazalendo na kuzidisha mjadala kuhusu ushindani wa nafasi ya urais kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

 

Membe ambaye pia alikuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya awamu ya nne, Julai 6 mwaka huu alirudisha kadi yake ya uanachama CCM baada ya Kamati Kuu ya CCM kuazimia kumfukuza uanachama Februari 28 mwaka huu kisha uamuzi huo kubarikiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Julai 10, mwaka huu.

 

Mwanadiplomasia huyo alipokelewa rasmi jana na wanachama wa ACT wazalendo waliokuwa wameambatana na viongozi wao katika ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam.

 

Miongoni mwa viongozi waliompokea Membe ni Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa chama hicho, Makamu wenyeviti wa chama hicho, Juma Duni Haji (Zanzibar) na Doroth Semu wa Bara.

 

Akizungumza ukumbini hapo, Membe alitoa rai vyama vya upinzani kuungana na kumsimamisha mgombea mmoja wa urais.

 

“Naomba nitoe wito kwa kambi za upinzani, ni lazima tuungane ili tuweze kumtoa mtu yule Ikulu, ili tumpeleke nyumbani akapumzike ili turekebishe haya mambo kama tunavyopanga kwenye mkataba wetu na wananchi.

 

“Ni vizuri kambi ya upinzani, mimi nimeingia ACT lakini kambi ya upinzani ni kubwa tukitaka tuchewele tusiende Ikulu shauri yetu, tukitaka tusiungane tusiende Ikulu shauri yetu, tuungane.”

 

 “Tuungane pamoja katika ngazi ya taifa, tuende kifua mbele kuchukua uongozi wa nchi ambao barabara iko wazi nina imani na viongozi wa ACT-Wazalendo watalibeba hili,” alisema Membe.

 

Huku akishangiliwa, Membe alisema amejiunga na ACT Wazalendo kuleta mabadiliko hasa ikizingatiwa kuwa chama hicho kinakua kwa kasi.

 

Aliongeza kuwa baada ya kujiunga ACT Wazalendo, hatoangalia nyuma kwa kurudi alipotoka kama ilivyotokea kwa Edward Lowassa.

 

Aidha, ujio wa mwanadiplomasia huyo umeendelea kuibua mjadala kuhusu nafasi ya urais baada ya kuombwa na Maalim Seif achukue fomu ya kuwania nafasi hiyo ndani ya chama hicho.

 

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wameutafsiri ujio wake ndani ya upinzani kuwa utazidi kunogesha mchuano wa urais.

 

“Kwa sababu Membe anayo makundi ya wanaCCM ambao watahamia upinzani kama alivyosema kuwa wapo zaidi 8000, lakini pia wapo wanaomuunga mkono kimyakimya.

 

“Kwa maana hiyo ujio wa Membe ni chachu kwa vyama vya upinzani kuleta ushindani wa kipekee, tofauti na ule wa 2015 lakini hali ya kisiasa sasa inaonesha Watanzania wanataka kuchagua mtu na sio chama tena,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk. George Khangwa.

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply