The House of Favourite Newspapers

Membe Amjibu Rostam: Wewe ni Mwenzetu Sote Tumekatwa Mkia

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe, amemjibu mfanyabishara Rostam Aziz kuhusu suala la kugombea urais 2020 akimtaka hivi sasa ajikite kwenye masuala ya kitaifa yanayohusu uchumi.

 

Membe ametoa kauli hiyo nje ya  Mahakama Kuu ya Tanzania, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kusikilizwa kwa kesi anayodai fidia dhidi ya mmiliki wa gazeti la Tanzanite, Cyprian Musiba, ambapo aliulizwa swali kuhusiana na kauli inayodaiwa kutolewa na mfanyabiashara Rostam Aziz juu ya uchaguzi wa mwakani.

 

Mei 16, 2019, picha moja ya video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimwonyesha Rostam akizungumzia suala la urais 2020 na kumshauri Membe asijitokeze kuwania nafasi hiyo badala yake aachiwe Rais John Magufuli kwa awamu nyingine.

 

Membe amesema: “Kuhusu kugombea mwakani napata kigugumizi kumjibu Rostam, lakini yeye ni mchumi na nitakutana naye nimshauri anafanya vizuri kwa Watanzania anapozungumzia masuala ya uchumi, inabidi azungumzie ‘main issue’ za nchi sio ‘personal’, hizi tunaachia watu wa chini.

 

“Kwa level (kiwango) yetu ni kuzungumzia masuala ya kitaifa na masuala ya kiuchumi, kwa nini uchumi wetu upo hapa ulipo? Kwa nini wafanyabiashara wanafunga biashara zao, Rostam ni economist (mchumi) namshauri aji-address (ajielekeze) kwenye masuala ya uchumi, Rostam wewe ni mwenzetu sisi tumekatwa mkia,” alisema Membe na kuongeza:

 

“Ukikatwa mkia hata ujitahidi vipi mkia wako ni mfupi tu, tunayoyazungumza ni vizuri tuwe ‘consistency’  (sambamba) mdomoni na dhamira yetu, Rostam ni mchumi mzuri sana, tuzungumzie masuala ya uchumi wa nchi yetu, kuliko kujaribu kuwa mtoto mzawa badala ya kukubali status (hadhi)…  Rostam na mimi ni watoto wa kambo.” alimalizia Membe.

Comments are closed.