The House of Favourite Newspapers

MEYA DAR AWAONYA WANAOUZA VIWANJA MABONDENI

0

 

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa kuepuka kujihusisha kwenye suala la uuzwaji wa maeneo yaliyopo mabondeni, yasiyopimwa na yenye migogoro.

Mwita amesema kuwa wenyeviti ndiyo wasimamizi wa maeneo hayo na kwamba wanapaswa kujiepusha na mambo hayo kwani kufanya hivyo ni kujiingiza kwenye migogoro isiyokuwa ya lazima na kuwasababishia wananchi kupata usumbufu wa mafuriko nyakati za mvua.

Kauli ya Mwita imekuja ikiwa ni baada ya kurejea jijini akitokea Ujerumani wiki moja iliyopita alipokuwa kwenye mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi uliohusisha mameya wote duniani na wataalamu wa masuala ya mabadiliko hayo.

Pia amefafanua kuwa wenyeviti wa serikali za mitaa ndiyo wanaosimamia makazi ya wananchi ikiwemo kushughulikia suala la upimaji na kwamba wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanaepuka kushiriki katika suala hilo la uuzwaji wa maeneo ambayo yana asili ya mikondo ya maji.

“Ni kweli kumekuwa na migogoro ya namna hii, sasa ni jukumu la kila kiongozi kwenye mtaa wake asikubali kujihusisha kwenye uuzwaji wa maeneo ambayo hayajapimwa na yaliyopo mabondeni, kwani kufanya hivi ni kujiletea matatizo kwao na kwa wananchi pia,” amesema.

Akizungumzia suala la upandaji miti, amesema kuwa wananchi wanapaswa kupanda miti kwenye maeneo wanayoishi na akasisitiza kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kuwa mfano kwenye maeneo yao.

“Suala la upandaji miti ni jukumu la kila mmoja, lakini katika jiji langu, niwaombe waandishi wa habari kuwa mfano kwenye hili, kwa kuwa nyinyi ndiyo kikoo cha jamii,” alisisitiza.

Alisema yeye amepanda miti kwenye eneo lake na ataendelea kufanya hivyo hadi kila mwananchi apate hamasa ya kufanya hivyo.

 

NA  DENIS MTIMA/GPL

Leave A Reply