The House of Favourite Newspapers

Mgambo Waliopiga Raia Dar Wafikishwa Kortini – Video

WANAODAIWA kuwa Askari Mgambo wawili Kelvin Sawala, Goodluck Tarimo ambao ni Askari Mgambo na ofisa Mtendaji kata ya Bunju, Ibrahim Mabewa (39), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kosa moja la kumshambulia na kumjeruhi kwa kutumia Rungu mkazi wa Bunju, Robinson Olotho.

Wakisomewa hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Mahira Kasonde, Wakili wa serikali, Mwanaamina Kombakono amedai washtakiwa wanakabiliwa na kosa moja la kusababisha majeraha. Washtakiwa hao wanadaiwa wametenda kosa hilo Agosti 30, mwaka huu maeneo ya Bunju ambapo walimpiga Robinson kwa kutumia rungu sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha.

Baada ya kusomewa kosa hilo washtakiwa wamekana kosa hilo, ambapo upande wa mashtaka umeeleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Wakili wa serikali, Nassoro Katuga amesema licha ya kesi hiyo kudhaminika lakini wanaiomba mahakama isubirishe dhamana ya washtakiwa hao kwa sababu kuu mbili.

Alitaja sababu hizo kuwa kwanza ni suala la kiusalama ambapo washtakiwa walionekana kwenye video zilizosambaa mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari, hivyo kama watapatiwa dhamana usalama wao utakuwa shakani kwa sababu wananchi na ndugu wa mjeruhiwa watakuwa na hasira. Sababu nyingine ni kwamba mjeruhiwa bado yupo hospitali na hali yake ya kiafya sio nzuri.

 

Hakimu alipowauliza watuhumiwa hao kuhusu hoja hizo walidai kuwa suala la usalama wao liko vizuri, hivyo wanaomba dhamana, pia kuhusu hali ya afya ya mjeruhiwa walionana naye jana na anaendelea vizuri wala hayupo hospitalini.

 

Katika uamuzi wake, Hakimu Kasonde amesema mahakama imekubali hoja za upande wa mashtaka kuhusu usalama wa washtakiwa hao, hivyo wananyimwa dhamana hadi hapo mahakama itakapojiridhisha kuhusu usalama wao.Kesi imeahirishwa hadi Septemba 20, mwaka huu.

 

NA DENIS MTIMA  | GPL

 

VIDEO: SHUHUDIA TUKIO HILO

Comments are closed.