The House of Favourite Newspapers

Mgombea Mwenza wa Trump Apata Ajali ya Ndege

mike-pence-3 Mr Pence (kati) azungumza na wazima moto LaGuardia

MAREKANI: Mgombea mwenza wa Donald Trump kupitia Chama cha Republican kwenye kinyang’anyiro cha urais nchini Marekani, Mike Pence amenusurika kifo baada ya ndege iliyokuwa imembeba kuteleza uwanja wa ndege.

Ndege hiyo iliteleza na kuvuka barabara inayotumiwa na ndege kupaa na kutua katika Uwanja wa LaGuardia jijini New York.

mike-pence-2Mike Pence (kati) atembea kutoka ndege iliyokuwa imembeba uwanja wa LaGuardia jijini New York

Pence ambaye pia ni Gavana wa Indiana amewaambia wanahabari kwamba yuko salama baada ya kisa hicho na hakuna mtu aliyejeruhiwa. Pia Bw Pence na abiria wengine takriban 30 waliokolewa kupitia mlango wa dharura wa ndege upande wa nyuma.

mike-pence-4 Ndege hiyo iliyombeba Pence hatimaye ilisimama kwenye maeneo yenye nyasi

Wakati anapata ajali hiyo, Pence alikuwa anatoka kwenye mkutano wa kampeni huko Fort Dodge, Iowa ambapo rubani wa ndege hiyo anadaiwa kukanyaga breki ghafla na baadaye abiria wanasema walihisi harufu ya taili ikiungua.

Kanda za video za runinga zimemuonesha Bw Pence baadaye akiwa amesimama kwenye mvua karbu na magari ya huduma za dharura, akizungumza na baadhi ya maafisa wa uokoaji na zimamoto.

mike-pence-1 Mike Pence alikuwa amepakia picha hii kwenye Twitter awali

Baadaye aliandika kwenye Twitter: “Nashukuru sana kwamba kila mtu aliyekuwa kwenye ndege yetu yuko salama. Nashukuru maafisa wa dharura na wote waliotuombea. Tutarejea kwenye kampeni kesho!”

Pia hakusita kueleza kuwa matope yaliruka na kujaa kwenye kioo cha sehemu ya mbele ya ndege.

Mgombea urais wa Chama cha Republican Donald Trump alimpigia simu Bw Pence kumjulia hali baada ya kisa hicho, maafisa wa kampeni wamesema.

Msemaji wa Trumo Stephanie Grisham alisema mgombea huyo alikuwa kwenye msafara wa kampeni akielekea Geneva, Ohio.

Bw Trump alizungumzia ajali hiyo kwenye mkutano wake wa kampeni baadaye akisema: “Mnajua, kulitokea ajali kubwa ya ndege.

“Ndege imeteleza kutoka barabara uwanja wa ndege na ilikaribia sana kuwa mbaya, kuwa mbaya sana, nimezungumza na Mike sasa hivi na yuko salama. Alitoka. Kila mtu yuko salama.”

Bw Pence aliahirisha hafla ya kuchangisha pesa ambayo ilifaa kuandaliwa katika jumba la Trump Tower eneo la Manhattan, na akaelekea moja kwa moja hadi hotelini.

Haijakuwa wiki njema kwa gavana huyo wa Indiana.

Jumatano, aliandika kwenye Twitter kwamba mbwa wake kwa jina Maverick, alikuwa amefariki akiwa na miaka 13.

Comments are closed.