The House of Favourite Newspapers

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 34

0

Si huyu mwenzetu ametobolewa utosi, chembechembe za ubongo ziko nje na mwili wake umekakamaa. Hapa chini ni damu tupu!”

 “Unasema kweli?” nikamuuliza kwa mshituko.

 Sikutaka kuinama kuitazama hiyo hali niliyoelezwa kwani yale maelezo tu tayari yalikuwa yameshanisisimua damu.

 “Inaelekea tulipoondoka, lile jini lilifika hapa likamfyonza damu huyu mwenzetu,” mwenzangu huyo akanieleza.

 “Mimi nadhani tunajitahidi tu lakini hatutabaki. Labda hili jini linatuzunguka ndiyo maana hatuoni pa kutokea, kila tukienda tunajikuta tumerudi tulikotoka na mwenzetu mmoja anauawa.”

 “Sasa unasikia,” yule mwenzangu aliniambia kisha akainuka.

 “Tuondoke,” akaniambia.

 “Tutaelekea upande gani?” nikamuuliza.

 “Kokote tu lakini tuondoke mahali hapa, linaweza kurudi tena kututafuta.”

“Huko tutakako kwenda tutajuaje kama hatutakutana nalo?”

 “Tusichukulie hivyo. Tujipe matumaini.”

 Ile njia iliyotufikisha pale ndiyo tuliyoitumia kurudi. Miguu yangu ilikuwa ikiendelea kuuma na kuvimba. Sasa nilikuwa nachechemea kama mgonjwa.

 Safari hii hatukutembea sana. Nilimwambia mwenzangu tupumzike. Tukapumzika. Kwa sababu ya kule kuchoka tulikuwa tunalala ovyo.

 Tulipokaa chini tu tukalala hapo hapo. Wakati nikiwa kwenye usingizi huo wa uchovu niliota mimi na wenzagu tunasafiri katika jahazi huku tunazungumza na kucheka. Ghafla hali ya hewa ikabadilika.

 Bahari ilichafuka. Jahazi letu likawa linasuasua na kujaa maji. Wenzangu walianza kujitosa baharini mmoja mmoja. Mimi na mwenzangu mmoja tukawa tumeng’ang’ania ndani ya jahazi hilo lililokuwa linazama.

 Ghafla jahazi likapasuka vipande viwili. Mimi nilikuwa nimeshika ubao wa upande mmoja wa jahazi hilo. Mwenzangu hakuwahi kushika chochote. Wakati anataka kutumbukia baharini niliwahi kumshika mkono.

Wakati huo  mwili wake wote ukiwa ndani ya maji.

Nikaendelea kumshikilia ili asizame hadi lilipokuja wimbi kubwa likamsomba na kumzamisha. Hapo hapo nikazinduka usingizini.

 Wakati nazinduka niliona purukushani upande wangu wa kulia ambapo alikuwa amekaa yule mwenzangu. Nikainuka na kuketi huku nikiangaza macho yangu.

Kumbe wakati tumelala Kaikush alikuja kimyakimya akamvamia yule mwenzangu. Ulikuwa ni wakati ule naota ile ndoto.

Jini huyo alifanikiwa kumsimamisha mwenzangu huyo na kumtoboa kwenye mshipa wa shingo yake na kumfyonza damu.

 Nilipoona hivyo nilinyanyuka haraka nikamsukuma Kaikush ili nipate nafasi ya kukimbia kuokoa maisha yangu.

 Miguu yangu ilikuwa mibovu lakini muda ule niliiona kama mizima. Ingawa nilikuwa nachechemea, niliweza kukimbia.

 Nilimsikia Kaikush akiniambia nyuma yangu.

“Wewe kimbia tu lakini hutaweza kutoka ndani ya pango hili. Na wewe nitakuua tu kwani nimeshajua umebaki peke yako.”

Maneno yale yalizidi kunitia hofu nikaendelea kukimbia huku nikijigonga na kuta za pango.

Kwa muda wa  dakika chache niliweza kwenda mbali sana. Ghafla nikaona waya mweupe umekatiza mbele yangu. Ulitoka katika njia iliyotoka upande wa kushoto kuelekea upande wa kulia.

Nikasimama na kujiuliza ulikuwa waya wa nini. Sikupata jibu. Nikainama na kuushika. Nikaona kweli ulikuwa ni waya kama wa umeme au wa simu.

 Nikajiuliza tena waya huo ulikuwa unatoka wapi na ulielekea wapi. Baada ya kushindwa kupata jibu nikauvuta upande mmoja. Nikahisi kama ulikuwa umeshikwa na mtu. Nikajitahidi kuuvuta tena, nikaona umelegea na ulikuwa unavutika kidogodogo.

Leave A Reply