The House of Favourite Newspapers

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 43

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Wewe ulimuona kwa macho yako huyo jini?”
“Ndiyo nilimuona”
“Yukoje?”

“Ni kama binadamu lakini anatisha.”
“Unajua ninakuuliza maswali mengi kwa sababu tukio lenu limehusisha vifo vya watu wengi. Kwa hiyo ni lazima tupate maelezo ya kina.”
SASA ENDELEA…

Kachero huyo aliendelea kuniambia.

“Tunataka tupate maelezo yanayoeleweka ili tuweze kuyaweka katika jalada la uchunguzi wa vifo vya watu wale. Na hata kama sisi wapelelezaji tunaulizwa nini kiliwaua watu wale, tuweze kuwa na majibu ya kuridhisha.”
Kachero huyo alipoona nimenyamaza akaniuliza.

“Sijui kama umenielewa?”
“Nimekuelewa,” nikamjibu.
“Kwa hiyo ni vyema utueleze kinaganaga kilichotokea ndani ya yale mapango tangu mlipoingia hadi mlipotoka.”

“Ni vilevile nilivyoeleza mwanzo,” nikamwambia.
“Bado unasisitiza kuwa wale watu waliuawa na jini?”
“Ndiyo, waliuawa na jini.”

Kachero huyo aliyejifanya kama msomi lakini hakuwa na lolote, alikunja uso wake akanitazama kwa ghadhabu.
“Mbona hatuelewani kaka?” akaniuliza.
“Unataka tuelewane kitu gani?”

“Sasa mimi nitaandika jini humu ndani ya jalada, wakuu wangu watanielewa kweli?”
Swali hilo likanifanya nihamaki.
“Sasa ulitaka uandike nini?” nikamuuliza kijeuri.
“Hilo siyo swali la kuniuliza.”

“Nimekuuliza hivyo kwa sababu nimekwambia watu hao wameuawa na jini, wewe unaniambia huwezi kuandika jini. Sasa andika unavyoona wewe.”
Nilipomwambia hivyo ndiyo alizidi kuhamaki.
“Wewe ulijuaje kuwa huyo kiumbe alikuwa ni jini, wewe unawajua majini, uliwahi kuwaona wapi?”

“Niliambiwa na yule msichana tuliyemkuta mle ndani kuwa yule kiumbe anayeua watu ni jini, sasa labda uende ukamuulize yeye alimjuaje!”
Kachero akawa hana tena swali akabaki kunitazama kwa uchungu huku akiinuka.
“Sawa,” akaniambia kwa hasira na kuondoka na wenzake.

Nilijiambia kama yule ndiye bosi wa wale wenzake, alitakiwa arudi upya kwenye chuo cha polisi kwani maswali yake hayakuwa na msingi na uelewa wake ulikuwa mdogo sana. Unaweza kubishana naye hata kwa kutwa nzima kwa jambo la kipuuzi tu.

Sikujua walikwenda kumuhoji nini Faiza kwani hawakurudi tena kwangu.
Nilikuwa nimeshapanga kama wangerudi tena nisingewapa maelezo yoyote kwa sababu nilijua tusingeelewana.

Asubuhi ya siku ya pili yake muuguzi mmoja aliniletea gazeti la siku ile akanionesha habari yetu ambayo iliandikwa katika gazeti hilo.

Ilikuwa ndiyo habari iliyopamba ukurasa wa mbele wa gazeti hilo ikiwa na picha moja kubwa iliyotuonesha mimi na Faiza tukiwa tumekaa mbele ya pango.
Niliitambua ile picha. Tulipigwa na waandishi wa habari mara tu tulipotoka katika pango hilo.
Macho yangu yalikutana na kichwa cha habari kilichosomeka;

WATU WALIOKWAMA KWENYE MAPANGO WATOKA
Chini ya kichwa hicho kulikuwa na vichwa vidogo vidogo vilivyosema.
“Ndani ya pango hilo akutwa msichana aliyekaa humo kwa miaka minne.”
“Wengine walioingia wadaiwa kuuawa na jini.”

“Utaniachia nisome?” nikamuomba yule muuguzi.
“Soma tu, mimi nimeshasoma.”
“Asante”

Nikakaa vyema na kuanza kuisoma ile habari. Jinsi walivyoiandika hawakuwa wameipatia sawa sawa lakini suala la Faiza lilifafanuliwa vizuri.
Gazeti lilieleza kuwa Faiza alipotea kwao Bagamoyo miaka minne iliyopita na kuja kujikuta yumo ndani ya mapango hayo ambamo ameweza kuishi kwa miaka minne bila kutoka nje.

Nilihisi waandishi walikuwa wakikwepa sana kulieleza kinagaubaga suala la Abdallah Kaikush ambalo tuliwaeleza wazi, kwamba ni jini na ndiye aliyemteka Faiza na kuwaua watu waliongia ndani ya pango hilo kwa kuwafyonza damu.
Baada ya kuisoma ile habari nilipata ahueni. Kwa vile picha yangu ilitolewa ndugu zangu wa Pemba wakiiona wanaweza kuja kuniona.

Siku ya tatu yake tukiwa bado tupo pale hospitali tukapata wageni ambao hatukuwatarajia. Ndugu wa familia ya Faiza walifika pale hospitali kutoka Bagamoyo.
Walifika Tanga baada ya kusoma ile habari iliyoandikwa kwenye gazeti ikiwa pamoja na picha iliyomuonesha Faiza na mimi.

Baada ya ndugu hao kuuliza walipelekwa katika wodi aliyolazwa Faiza.
Faiza alifurahi kuwaona ndugu zake na ndugu hao walifurahi kumuona ndugu yao akiwa hai.

Faiza mwenyewe pamoja na baadhi ya ndugu zake hao walitiririkwa na machozi ya furaha baada ya kukutana tena. Baada ya kuzungumza kwa kirefu, Faiza aliwaleta ndugu zake katika wodi niliyokuwa nimelazwa.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave A Reply