The House of Favourite Newspapers

Michirizi Ya Damu – 01

0

GIZA, Misri     

Zilisikika kelele kutoka ndani ya piramidi moja lililokuwa katika Mji wa Giza uliokuwa nchini Misri. Watu waliokuwa humo ambao asilimia kubwa walikwenda kutalii wakatoka huku wakikimbia kwani mbali na kelele hizo, piramidi hilo halikuwa la kawaida, lilikuwa linatisha kiasi kwamba hata watalii waliokuwa wakiingia, walishikana mikono kama njia mojawapo ya kutokutana kuuawa na majini yaliyosadikiwa kwamba yalikuwepo ndani ya piramidi hilo.

Mwanamke yule aliyekuwa amepiga kelele akatoka huku akitetemeka, kijasho chembamba kikimtoka, walinzi waliokuwa mahali hapo wakamsogelea kwa lengo la kutaka kufahamu kilichomfanya mpaka kupiga kelele kiasi hicho hadi kuwaogopesha watu wengine.

Walipomuuliza mwanamke huyo wa Kiingereza akawaambia kwamba aliiona maiti ndani ya piramidi hilo kitu kilichomtisha kila mtu.

“What?” (nini?) aliuliza mwanaume mmoja.

“A deadbody!” (maiti)

“Are you sure?” (una uhakika?)

“Yes!” (ndiyo) alijibu mwanamke huyo huku akiendelea kutetemeka kwa hofu.

Watu wote waliotoka ndani ya piramidi hilo wakaanza kumwangalia mwanamke yule, wengine hawakuridhika, wakamsogelea na kumuuliza kilichokuwa kimetokea ndani ya piramidi lile, hakuficha, aliwaambia wazi kwamba aliiona maiti ikiwa chini kitu kilichomfanya kupiga kelele na kukimbia.

“Siyo kwamba umeona mauzauza?” aliuliza jamaa mmoja.

“Kwani mauzauza siyajui? Nimeona maiti!”

“Sasa kwa nini ulikuwa peke yako na wakati hairuhusiwi?” aliuliza mwanaume mwingine.

“Niliingia na mume wangu! Yeye alikwenda upande mwingine na mimi kwenda mwingine,” alijibu mwanamke huyo na mumewe kutokea hapo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumkumbatia mkewe.

Walinzi waliokuwa hapo wakachukua tochi zao na kuingia ndani ya piramidi hilo, walitaka kuona kile alichokiona mwanamke huyo. Kwa miaka mingi, tangu karne ya ishirini ilipoingia hakukuwa na mtu yeyote aliyekufa ndani ya piramidi hilo japokuwa kulikuwa na tetesi za kuwepo kwa majini. Kama hakukuwa na mtu aliyekufa! Iliwezekanaje mwanamke huyo kuona maiti humo?

Wakaingia mpaka ndani, wakaanza kumulika huku na kule, wakaelekea kule mwanamke yule alipokwenda huku wakiwa makini kuangalia chini. Kama alivyosema mwanamke yule ndivyo walivyokuta, macho yao yakatua katika mwili wa mwanaume mmoja uliokuwa chini, ulichomwa visu mara tatu kifuani na tumboni, mbali na hivyo, maiti yake iliburuzwa na kuachwa michirizi ya damu pale chini.

Kila mmoja alishtuka, hawakuamini kile kilichotokea, ilikuwaje mwanaume huyo auawe ndani ya piramidi hilo halafu muuaji asionekane? Kitu cha kwanza kabisa, hawakuigusa maiti ile, wakatoka ndani na kuelekea katika kompyuta zao na kuangalia orodha ya watu walioingia ndani ya piramidi lile dakika chache zilizopita kwani hata maiti ile ilivyoonekana, haikuonekana kama iliuawa muda mrefu uliopita.

“Mmeangalia jina lake?”
“Hapana!”
“Hebu kampekueni, mnaweza kuona hata kitambulisho,” alisema mwanaume aliyeshika kompyuta mpakato na hivyo walinzi hao kurudi ndani ya piramidi lile huku watu wengine wakiwa nje na idadi kubwa ya watu ikizidi kuongezeka.

Walipoingia humo, wakampekua mfukoni na kukuta ‘business card’ iliyomtambulisha kwa jina la Benjamin Keith, mwanaume wa Kimarekani aliyekuwa akimiliki kampuni kadhaa ikiwemo kampuni ya mavazi ya Cotton Keith.

“Kumbe ni Keith!” alisema mwanaume mmoja kwa mshangao.

“Ndiye nani?”
“Yule bilionea wa Kimarekani!”
“Unamaanisha yule mwenye utajiri wa dola bilioni kumi na mbili?” aliuliza mlinzi mwingine.

“Ndiyo!”
“Mh! Hebu nione hiyo kadi.”

Akakichukua na kuanza kukiangalia, kama alichokiona mwenzake na yeye alikiona hivyohivyo. Kila mmoja alishangaa, hawakuamini kile walichokuwa wakikiona, waliwafahamu sana matajiri, kila kona walipokuwa wakienda, walikwenda na walinzi wao, ilikuwaje Keith aende huko peke yake mpaka kuuawa? Kila walipojiuliza wakakosa majibu.
Wakatoka nje wakiwa na ile kadi na walipomuonyeshea jamaa aliyekuwa na kompyuta, akaangalia jina lile, akagundua kwamba Keith alikuwa ameingia ndani ya piramidi lile na msichana, mrembo aliyeitwa kwa jina la Maria Ogabugu aliyekuwa na asili ya Nigeria.

“Aliingia na mwanamke humu ndani,” alisema jamaa huyo.

“Hebu tuone.”

Akaangalia kwenye kompyuta ile kwa lengo la kujiridhisha, kile alichoambiwa ndicho alichokiona kwamba bilionea huyo aliingia na mwanamke aliyejulikana kwa jina hilo ndani ya piramidi hilo. Hawakujua mwanamke huyo alikuwa wapi kwani walikuwa na uhakika kwamba yeye ndiye aliyemuua Keith na kisha kukimbia.

Wakawasiliana na polisi ambapo baada ya dakika kadhaa wakafika na kuingia ndani ya piramidi lile. Wakaelekea mpaka kule kulipokuwa na maiti ile kisha kuiangalia. Ilionyesha kwamba hakuuawa muda mwingi uliopita, na hata kama muuaji alikimbia, hakuwa amefika Cairo.

Wakaupiga picha mwili ule kisha kuubeba kwa lengo la kuondoka nao ila kabla hawajaondoka, wakaona kipande cha karatasi kikiwa chini, kilikuwa kimezibwa na mwili ule, wakakichukua kikaratasi hicho kilichoandikwa kwa maneno machache kwa Kifaransa yaliyosomeka C’est fait yakiwa na maana ya kukamilika kwa jambo au ‘done’ kwa Lugha ya Kiingereza.

Hilo likaibua maswali mengi, hakukuwa na mtu aliyejua maana ya neno lile lililoandikwa. Mwili ukachukuliwa na kupelekwa hospitali ambapo familia yake ikapigiwa simu na kuambiwa kile kilichokuwa kimetokea.

Taarifa hiyo ikawekwa kwenye mitandao ya kijamii na kutangazwa sana katika vituo vya televisheni na radio. Kila mtu aliposikia habari hiyo alishangaa, hawakuamini kama bilionea Keith aliuawa ndani ya piramidi nchini Misri kwani alikuwa mtu mwema ambaye kila mtu alijua kwamba angeishi miaka mingi kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia watu masikini.

Serikali ya Marekani haikutaka kukubali, mawasiliano yakafanyika kwenda nchini Misri na kuwaambia kwamba wafanyaje kila linalowezekana mpaka muuaji huyo apatikane, kama walikuwa na uwezo wa kwenda sehemu yoyote ile, ilikuwa ni lazima mwanamke huyo akamatwe.

Lilikuwa ni agizo kubwa na gumu, hawakujua mahali alipokuwa muuaji hivyo polisi kwenda kuulizia katika piramidi hilo na kuambiwa kwamba bilionea huyo alikuwa na mwanamke wa Kinageria aliyeitwa Maria Ogabugu.

“Huyu mwanamke ndiye anayetakiwa kutafutwa na kupatikana haraka iwezekanavyo,” alisema kamanda wa jeshi la polisi jijini Cairo.
“Sawa mkuu!”

Usikose sehemu ya pili hapa siku ya kesho.

Leave A Reply