The House of Favourite Newspapers

Mitambo Imewashwa Ligi Kuu Bara Leo Jumapili

0

MITAMBO imewashwa kwa ajili ya msimu wa 2020/21 ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo leo Jumapili kutakuwa na jumla ya dakika 540 zitashuhudiwa timu 12 zikitoana jasho viwanjani.Dakika hizo 540 ni sawa na mechi sita, kisha kesho Jumatatu zitachezwa dakika nyingine 270 kwa mechi tatu kukamilisha raundi ya kwanza yenye jumla ya mechi tisa.

 

Leo na kesho, tutashuhudia hekaheka hizo kwa dakika 810 ambapo ndipo zitakuwa zimechezwa mechi zote tisa na timu 18 kushuka dimbani.Usajili uliofanywa na timu zote 18 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu kuanzia Agosti Mosi hadi 31, mwaka huu, leo ndiyo tutaanza kuona matunda yao, nani amefanikiwa na nani amefeli.

IHEFU VS SIMBA

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba watakuwa ugenini mkoani Mbeya kucheza na wageni kunako kwenye ligi, Ihefu. Mchezo huu unatarajiwa kuanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

 

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema wachezaji wake wapo tayari kwa kuibuka na ushindi.Wakati kocha akizungumza hivyo, mashabiki wa Simba, wamekiangalia kikosi chao kilichosheheni mastaa akiwemo Larry Bwalya, Bernard Morrison na Clatous Chama, wakaibuka na kusema: “Kwa kikosi hiki, tupeni kombe letu mapema.

Kumbuka timu hizi zinakutana kwa mara ya kwanza jambo ambalo limemtia hofu Sven na kukiri wazi kwamba alilazimika kukesha ili kusoma mbinu za wapinzani wao hao, na tayari amezifahamu, hivyo hana presha.

YANGA VS PRISONS

Wakati Simba wakiwa Mbeya, watani zao wa jadi, Yanga watajitupa nyumbani kwenye Dimba la Benjamini Mkapa jijini Dar kuikaribisha Prisons ya Mbeya.Yanga imekuwa na rekodi nzuri mbele ya Prisons kwani tangu mwaka 2013 zilipokutana kwenye ligi hadi sasa, Yanga imeshinda mechi kumi na kupoteza moja, huku sare zikiwa tano.

 

Rekodi hiyo inawapa kiburi Yanga, lakini pia uwepo wa mastaa wapya wakiwemo Carlos Carlinhos, Farid Musa, Tuisila Kisinda na Bakari Mwamnyeto, wenyewe wanatamba wakisema: “Tulieni wapinzani, huu ubingwa ni wetu.

”Kwa misimu mitatu mfululizo tangu Yanga ilipobeba taji la Ligi Kuu Bara 2016/17, imeshuhudia taji hilo likienda Simba, hivyo safari hii wameamua kuleta mapinduzi.Yanga na Prisons zilipokutana msimu uliopita ndani ya Ligi Kuu Bara, ilishuhudiwa Yanga ikiwa na matokeo mazuri zaidi, ilishinda moja na sare moja. Haikupoteza. Mechi inatarajiwa kuanza saa 1:00 usiku.

 

NAMUNGO VS COASTALWawakilishi wa kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, Namungo, wataanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi kucheza na Coastal Union. Mechi itaanza saa 8:00 mchana.Namungo na Coastal zilipokutana msimu uliopita uwanjani hapo, Coastal waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, hivyo leo Namungo watakuwa na muda wa kujiuliza ilikuwaje siku ile wakachapwa nyumbani.Ikiwa tayari timu hizo zimekutana mara mbili, Coastal imeshinda moja na sare moja. Namungo haijaonja ushindi.

 

MTIBWA VS RUVU

Mtibwa wataikaribisha Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Gairo uliopo Morogoro. Mara ya mwisho timu hizo zilikutana uwanjani hapo kwenye mechi ya kumaliza msimu wa 2019/20 na wenyeji kushinda kwa mabao 2-1. Mechi itaanza saa 10:00 jioni.Mechi zingine leo ni Biashara United vs Gwambina kwenye Uwanja wa Karume mkoani Mara kuanzia saa 10:00 jioni na Dodoma Jiji vs Mwadui, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mechi itaanza saa 8:00 mchana.Baada ya leo kuchezwa mechi sita, kesho Jumatatu zitachezwa mechi tatu.

 

KMC VS MBEYA CITY

Kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar, wenyeji KMC watapambana na Mbeya City, mechi ikianza saa 8:00 mchana. Matokeo yao msimu uliopita yalikuwa hivi; Mbeya City 0-1 KMC na KMC 0-3 Mbeya City.

 

KAGERA VS JKT TANZANIA

Kagera Sugar watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera kupambana na JKT Tanzania. Mechi itaanza saa 10:00 jioni. Msimu uliopita, JKT Tanzania ilishinda mechi zote nyumbani na ugenini kwa ushindi wa 1-0.

 

AZAM VS POLISI TANZANIA

Azam watafunga dimba kwa kucheza na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar kuanzia saa 1:00 usiku. Azam wana kumbukumbu nzuri dhidi ya Polisi Tanzania kwani msimu uliopita ilishinda mechi zote mbili kwa matokeo ya 1-0.Azam ambao wengi kama wamewatoa kwenye ushindani wakizipa nafasi kubwa Simba na Yanga, wenyewe wanawaangalia tu, kisha wanasema: “Tutawashangaza msimu huu.

 

”Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’, amesema: “Ukiangalia usajili ambao tumeufanya kwa ajili ya msimu huu, utagundua kuwa tumeijenga timu yetu katika misingi ya kushindania ubingwa. Hivyo tunautaka ubingwa.

 

”WAAMUZI SASA SAFI

Wakati ligi ikianza leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Sudi Abdi, amesema dosari zote zilizoonekana msimu uliopita zimefanyiwa kazi.Hiyo ni baada ya msimu uliopita baadhi ya waamuzi kutupiwa lawama za kushindwa kutafsiri vema sheria 17 za soka, hadi wengine kufungiwa.Mwenyekiti huyo ameliambia Spoti Xtra kwamba: “Tumewapa semina waamuzi kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya vizuri katika ligi ili kuondoa dosari zilizoonekana kwa msimu uliopita na upande wa malipo yao yataenda vizuri.”

Leave A Reply