The House of Favourite Newspapers

Mkazi wa Makoroboi Mwanza Apandishwa Kisutu Kwa Tuhuma za Wizi

0

MFANYABIASHARA, Krushna Karia (37) Mkazi wa Makoroboi jijini Mwanza, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za wizi wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 284.8 alivyopewa na Kiwanda cha Cello kwa malengo ya kibiashara.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa mshtakiwa ana tuhuma kwa kosa moja la wizi.

Wakili Nguka amedai Karia anatuhumiwa kutenda kosa halo kati ya Mei 19 na Septemba 21, 2018, ambapo anadaiwa kuiba  bidhaa mbalimbali ikiwemo viti, stuli, majagi, vikapu, majaba, ndoo.

Aliendelea kudai kuwa, bidhaa zingine ni vifungashio vya chakula,  ndoo za takataka , vikombe na mabeseni, vyote vikiwa na thamani ya Sh 284,845,702 alivyopewa na Kiwanda cha Cello kwa madhumuni ya kibiashara.

Baada ya mshtakiwa huyo, kusomewa makosa yake alikana kutenda mashtaka hayo, ambapo Wakili Ngukah alidai upelelezi unaendelea na upande wa mashtaka hauna pingamizi juu ya dhamana ya mshtakiwa.

Hakimu Shaidi alisema ili mshtakiwa awe nje kwa dhamana anatakiwa awe na wadhamini wawili, wenye vitambulisho vya Taifa au taasisi inayotambulika, mmoja asaini bondi ya Sh milioni moja na mwingine awasilishe hati ya mali isiyohamishika.

Pia, mshtakiwa anaweza kuwasilisha fedha taslimu nusu ya jumla ya thamani ya mali anayodaiwa kuiba.

Mshtakiwa hakuweza kutimiza  masharti hayo, ambapo amerudishwa rumande hadi Juni 10 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Leave A Reply