The House of Favourite Newspapers

Mke Akimbia Kuchinjwa Kafara la Utajiri

mama-akimbia-kuchinjwa-kafara-la-utajiri-1 Stori: Gladness Mallya na Hamida Hassan | Gazeti la Uwazi, Toleo la Desemba 27, 2016

Dar es Salaam: Ni tukio baya la kufungia mwaka 2016! Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Mariam Chacha Maruambura, aliyesema ni mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu ametoroka nyumbani kwake na kukimbilia jijini hapa akidai kwamba kuna nduguye (jina linahifadhiwa) anataka kumtoa kafara ya utajiri.

Awali, Uwazi lilisimuliwa mkasa wa mwanamke huyo na baadaye kufanikiwa kuonana naye ana kwa ana Alhamisi iliyopita nje ya Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu Kinondoni, Mwananyamala, Dar.

MAHOJIANO NA UWAZI

Katika mahojiano na gazeti hili, Mariam alisema kwamba, aliamua kutoroka nyumbani kwake Bariadi na kumwacha mumewe, kisha yeye kufika Dar kwa ajili ya kuwatafuta ndugu wa mama yake ambao mmoja wao alimtaja ni msanii maarufu wa Muziki wa Taarab nchini (jina hatulitaji kwa vile gazeti halikumpata) kwa sababu mtu huyo aliyemkimbia alitaka kumuua kwa kumchinja ili kumtoa kafara.

Mariam alisema mtu huyo anayeisaka roho yake kwa kumwambia ‘laivu’ ana utajiri hivyo kutaka kutolewa kafara, anaamini ni kwa ajili ya mambo ya utajiri jambo ambalo yeye hakukubaliana nalo na hivyo kuamua kuisalimisha roho yake.

mama-akimbia-kuchinjwa-kafara-la-utajiri-2

Mariam Chacha Maruambura akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kinodnoni, Dar, Ally Hapi.

KUMBE ANA MUME

Mariam alisema kuwa, aliolewa mwaka 2004 na mwanaume aliyemtaja kwa jina moja la Masanja na wamejaliwa kupata watoto watano huku wakimiliki ng’ombe 1,000. Hata hivyo, Mariam hakusema ni namna gani, mumewe huyo alimsaidia kwenye sakata hilo la yeye kutaka kutolewa kafara.

ALIWAHI KWENDA KUWAAMBIA WAZAZI

“Kuna wakati nilijaribu kufika hadi nyumbani kwa wazazi wangu na kuwasimulia kuhusu mtu huyo lakini kaka zangu waliingilia kati na kusema hakuna msaada ninaoweza kuupata.

“Kwa kweli nimeteseka sana, ndiyo maana nikaamua kuja hapa Dar es Salaam kumtafuta (anamtaja msanii) maana ni ndugu yangu.”

ALICHOKUTANA NACHO ALIPOFIKA DAR

‘‘Nilifika Dar es Salaam, Desemba 17, mwaka huu, nikaulizia pale Stendi ya Ubungo (mabasi ya mkoani), kaka mmoja akasema anapajua anapoishi msanii huyo, tukapanda naye kwenye daladala ili anipeleke.

“Tuliposhuka, tukafika sehemu moja yenye uchochoro, cha ajabu yule kaka alinitolea kisu na kuninyang’anya simu na begi langu la nguo huku akiniambia nikipiga kelele ataniua.”

ally-hapiMkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Hapi.

MATESO BAADA YA HAPO

“Nina mtoto mchanga lakini hata nguo ya kumbadilisha sina maana zote zilikuwa kwenye begi lililoibwa, ilibidi baada ya kufanyiwa ukatili huo nisaidiwe na wasamaria wema na kurudi Stendi ya Ubungo. Nikawa nalala pale, wasamaria wema wakanisaidia kumpigia simu ndugu yangu msanii na wadogo zake, lakini nilipoongea nao walisema hawanijui.”

AONANA NA MKUU WA WILAYA KINONDONI

‘‘Wakati nikitafuta msaada ndipo nikasikia Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (Ally Hapi) anakuja Hospitali ya Mwananyamala ndiyo nikaja anisaidie angalau nauli nirudi tu nyumbani maana naona nitakufa, bora nikafie kwetu hukohuko,’’ alisema Mariam.

MKUU WA WILAYA AOKOA JAHAZI

Uwazi ndiyo lilimchukua Mariam na kumpeleka kwa Mkuu wa Wilaya, Ally Hapi kupitia kwa Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff), Simon Mwakifwamba.

Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa sasa, Alhamisi iliyopita alikuwa mgeni rasmi kwenye zoezi la Chama cha Wanawake wa Tasnia ya Filamu za Kibongo kuchangia damu, aliokoa jahazi ambapo baada ya Mariam kumweleza tatizo lake aliondoka naye kwenye gari lake kwa lengo la kwenda kumkatia tiketi na kumpa fedha za chakula ili arudi nyumbani kwake.

KAULI YA MKUU WA WILAYA

‘‘Pole sana. Siwezi kukupa fedha mkononi maana sina uhakika kama unadanganya au ni kweli hivyo kama unahitaji kurudi kwenu, panda kwenye gari langu mpaka ofisini kwangu, nitamtuma mtu akupeleke Stendi Ubungo, akupandishe basi la kwenu na fedha ya kula njiani,’’ alisema mkuu huyo wa wilaya akimwambia Mariam ambaye alipanda kwenye gari lake na kuondoka naye.

IMANI ZA MAKAFARA

Bado kuna mila potofu kutoka kwa baadhi ya makabila au watu ambao huamini kuwa, kumchinja binadamu, hasa ndugu au mtu anayekuhusu na damu yake kumwagika kwa ajili ya mizimu kunaweza kuleta utajiri jambo ambalo si kweli na linasababisha utengano katika jamii.

Ni mara nyingi viongozi wa dini wamesikika wakikemea imani potofu za makafara katika jamii, kwani nyingi zinanyima haki ya mtu kuishi kwa amani.

 

SHEHE MKUU DAR

Uwazi lilimtafuta Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum na kumsimulia kuhusu mkasa huo ambapo alisema anampa pole mwanamke huyo lakini pia analaani watu wanaotafuta utajiri kwa njia ya ushirikina.

“Huo ni ushirikina. Ni vizuri sana kama jamii ikamrudia Mungu kwa kumcha. Ikifanya hivyo, hayo mambo hayawezi kuwepo kamwe,” alisema shehe huyo.

MAMA RWAKATARE

Naye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Mlima wa Moto Assemblies of God Mikocheni B, Mama Getrude Rwakatare akizungumzia kadhia za makafara alisema:

“Hiyo yote ni watu kutokuwa na hofu ya Mungu. Watu wakimjua Mungu inatosha kabisa kuachana na tabia hizo ambazo ni machukizo mbele ya Mungu.”

 

Nay wa Mitego Ametoboa Siri: Hiki ndicho Alichokimiss kwa Shamsa Ford

Comments are closed.